Watu
wenye ulemavu nchini wamesema hatua zisizoridhisha zinazochukuliwa na
serikali dhidi ya vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na
wengine kusababishiwa ulemavu wa kudumu zinawasukuma kuishtaki serikali
kwenye umoja wa mataifa ambako serikali imeridhia na kusaini mikataba
yote ya kimataifa ya kumlinda mtu mwenye ulemavu.
Tamko hilo la watu wenye ulemavu linatolewa jijini Arusha na wadau
waliokutanishwa na program ya jumuiya ya makanisa duniani
inayoshughulikia utetezi wa watu wenye ulemavu kujadili ujumuishaji wa
watu wenye ulemavu katika nyanja za maendeleo.
Akizungumzia mauaji hayo katibu wa shirikisho la watu wenye ulemavu
nchini Bwana Felician Mkude anasema ni jambo la kushangaza kuona kuwa
serikali imekua ikielekeza nguvu kubwa pale wanyamapori wanapouawa
tofauti na mauaji ya watu wenye Albinism yanapotokea, lakini akaenda
mbali zaidi na kuzungumzia nguvu kubwa iliyoelekezwa kuwashughulikia
majambazi waliojitokeza jijini Tanga hivi karibuni akihoji ni kwa nini
nguvu hiyo hailekezwi kwa kundi hilo lililokosa amani.
Kwa upande wao wanaharakati wa haki za watu wenye ulemavu kutoka
asasi ya sasa foundation Bi Jovita Mlay na Bi Mackrine Rumanyika
wakazungumzia umuhimu wa jamii yote kushiriki kuwalinda watu wenye
ulemavu kwa kuanzia ngazi ya familia.