WAKATI Jeshi la Polisi likilaumiwa kutokana na namna
lilivyoshughulikia maandamano ya Chama cha Wananchi (CUF) wiki
iliyopita, Serikali imetahadharishwa kuwa makini na harakati za kisiasa
zinazotumia mbinu za kuchokoza Jeshi la Polisi na kuvunja sheria halali.
Wakizungumza na gazeti hili wiki hii kuhusu dhana ya udhaifu wa jeshi
hilo, baadhi ya watu wakiwemo wasomi wameitaka Serikali kuwa makini na
kauli za wanasiasa, ambao wamewahi kushiriki au kutoa matamko ya
kihalifu na leo wanatuhumu jeshi hilo.
Baadhi ya matukio ya kihalifu yaliyotajwa kufanywa katika mazingira
ya siasa, tamko la maandamano na migomo isiyokoma, bila kibali cha
Polisi, lililotolewa hivi karibuni na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa,
Freeman Mbowe na udhalilishwaji wa Mkuu wa Wilaya, wakati wa uchaguzi
mdogo wa Igunga uliokuwa na ushindani wa kisiasa mwanzoni mwa 2011.
Tahadhari hiyo imetolewa, wakati Serikali ikielezea kuridhishwa na
kazi ya kutunza amani nchini inayofanywa na jeshi hilo, na kuagiza
lijiandae na siasa za 2015; siasa za kabla ya Kura ya Maoni ya kupata
Katiba Mpya na za kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Maandamano ya CUF
Akitoa tamko kuhusu kudhibitiwa kwa maandamano ya CUF wiki iliyopita,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, akizungumzia hoja ya
mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia (NCCR- Mageuzi), kuhusu polisi
walivyodhibiti maandamano ya CUF, alisema Profesa Ibrahimu Lipumba,
ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alikaidi zuio la Jeshi la
Polisi.
Akifafanua zaidi, Chikawe alisema Januari 26 mwaka huu, Jeshi la
Polisi lilipokea barua kutoka CUF, iliyokuwa ikitoa taarifa za kufanyika
kwa maandamano kwenye viwanja vya Zakhiem Mbagala, Dar es Salaam.
“Maandamano yalipangwa kuanzia Temeke kwenda Zakhiem… Jeshi la Polisi
liliwaita viongozi wa CUF kwa mazungumzo. Walifanya mazungumzo na Jeshi
la Polisi lililotoa tahadhari kadhaa kutokana na sababu za kiusalama,”
alisema Chikawe.
Pamoja na CUF kuonekana kama vile walielewa tahadhari hiyo, Chikawe
alisema walishangazwa kuona Profesa Lipumba akikaidi zuio la Jeshi la
Polisi na kuamrisha wananchi kuandamana kuelekea Zakhiem.
“Jeshi la polisi linataka kila mtu kutii sheria bila shuruti, na mtu
yeyote akishindwa kufanya hivyo, Jeshi la Polisi litamshughulikia mtu
bila kujali umri, jinsia, wala madaraka yake,” alieleza Chikawe kuonesha
namna Lipumba alivyokaidi amri ya Polisi katika harakati hizo hizo za
siasa za ushindani.
Dk Bana
Akizungumza na gazeti hili jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), katika masuala ya Utawala na Siasa, Dk Benson Bana,
alishangaa Bunge kutumia fedha za umma, kujadili tukio la kiongozi mmoja
katika jamii aliyevunja sheria.
“Tuna viongozi wengi kuanzia wa kiroho, wa kiutamaduni na wa kisiasa,
inakuwaje kiongozi mmoja wa kisiasa akivunja sheria Bunge likae
kujadili?” alihoji, akizungumzia mjadala wa Bunge kuhusu kukamatwa na
kufikishwa mahakamani kwa Profesa Lipumba.
Aliwataka Watanzania kuwa macho na mbinu zinazotumika za kuchokoza
vyombo vya dola na kukumbusha kuwa kuna chama kimoja, ambacho hakukitaja
jina, lakini ni Chadema, kilichotoa tamko la kuhakikisha nchi
haitawaliki mara baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
“Yapo matamko mengi tu, lipo hata la Mbowe la maandamano na migomo
isiyokoma na katika matamko yote hayo, sijasikia siku hata moja vyama
vya upinzani vikisema Jeshi la Polisi linafanya kazi vizuri. “Kama
unajua siasa za Tanzania, suala la kuchokozwa Polisi ni la kawaida
lakini ni vyema vyombo vya habari vitusaidie, Polisi si chombo cha siasa
ni cha amri, hakipaswi kuchokozwa… sisi tunalala usiku na kuamka salama
dhamana ya usingizi wetu tunawapa wao,” alisema.
Akielezea namna wanasiasa wanavyopenda kuchokoza Polisi na vyombo
vingine vya dola, alitoa mfano wa baadhi ya wanasiasa kusimamisha
walinzi binafsi nyuma yao, wakati wakihutubia mikutano ya hadhara.
“Umeona katika nchi gani mwanasiasa anasimamisha mlinzi nyuma kama
Rais, wanajifananisha na Rais? Hii ni hadaa, hawa wamelewa madaraka
ambayo hawana,” alisema na kusisitiza umuhimu wa jamii kuelimishwa ili
wanasiasa waache kupima nguvu na vyombo vya dola.
Mbowe
Moja ya matamko ya kuchokoza Polisi, ni lililowahi kutolewa na Mbowe
la kufanya maandamano na migomo isiyokoma nchi nzima, mwishoni mwa mwaka
jana wakati wa Mkutano Mkuu wa Chadema.
Mbowe aliyekuwa akiomba kuchaguliwa katika nafasi hiyo kwa mara ya
tatu mfululizo, na hivyo kuvunja utamaduni wa chama hicho wa tangu
kilipoasisiwa, kwa kiongozi kuongoza kwa muda usiozidi vipindi viwili
vya miaka mitano, alitoa tangazo hilo kushinikiza kuvunjwa Bunge Maalumu
la Katiba.
“Natangaza azimio la Mkutano Mkuu ni kushirikisha umma kwa maandamano
na migomo kwa kibali cha polisi na bila kibali...siko tayari kwa
mazungumzo tena, nchi haiwezi kubadilika kwa mazungumzo ambayo ni
kuchezea fedha za umma. “Najua watatumia nguvu na kututisha na silaha za
moto. Lakini sisi tutasonga mbele,” alisema na kutaka kuundwe mtandao
wa Chadema na wananchi kushirikiana na Ukawa kila wilaya, kufanya
maandamano na migomo hiyo.
Aidha, aliagiza wanasheria wote wa Ukawa wakutane na kuona uwezekano
wa kufungua kesi dhidi ya wajumbe wa Bunge hilo, kuwashambulia kisiasa
wajumbe ambao ni wabunge katika majimbo yao ili kuhakikisha hawarejei
tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Pongezi za Serikali
Wakati mbinu hiyo ya kisiasa ikijionesha hadharani, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed,
amelitaka Jeshi la Polisi nchini kujipanga kukabiliana na vurugu za
kisiasa za 2015.
Mohammed Aboud, ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema vurugu
hizo zimeanza kuonekana wakati nchi ikielekea kwenye upigaji Kura ya
Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu.
Alisema hayo juzi jioni wakati akifunga mkutano wa maofisa wakuu
waandamizi wa Jeshi la Polisi uliokuwa ukifanyika mjini Dodoma, na
kuongeza kuwa Serikali imeridhika na utendaji wa Jeshi la Polisi katika
kuimarisha amani na usalama katika nchi.
“Sasa si tu suala la uhalifu, harakati za kisiasa husababisha kupotea
kwa hali ya usalama na kuleta vurugu… ni lazima kutengeneza mikakati ya
kukabiliana na hali hiyo,” alisema.
Alifafanua kuwa mikakati itakayowekwa, inapaswa iwe kwa ajili ya
kusaidia kufanikiwa kwa Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu, ili shughuli
hizo muhimu kwa mwaka huu, zifanyike kwa usalama na utulivu.
“Mjipange mapema na kujitayarisha na rasharasha zinazoonekana ili
wakati utakapofika, mkabiliane na hali halisi na Serikali itafanya kila
linalowezekana kulinda amani iliyopo,” alisema Alisisitiza licha ya
askari Polisi kufanya kazi katika mazingira magumu, lakini wamekuwa na
bidii katika kuhakikisha Taifa linakuwa katika hali ya usalama na kuipa
Tanzania sifa ya kuwa kisima cha amani.
Udhaifu wa Polisi
Hata hivyo akizungumzia dhana ya udhaifu wa Jeshi hilo, Mohammed
Aboud alisema katika Jeshi hilo kuna wakorofi wachache ambao kwa njia
moja au nyingine wanalitia doa Jeshi hilo.
“Lazima viongozi wa Jeshi muwe na utaratibu wa kutengeneza njia ya
kuwashughulikia wanaoharibu jina la jeshi ili waache tabia hiyo na
wachukuliwe hatua kabla ya kuharibu,” alisema.
Alitaja baadhi ya mambo yanayolalamikiwa sana kuwa ni unyanyasaji wa
vijana, kubambikia kesi, kutoa siri za raia, kuchelewesha upelelezi,
kutofika kwa wakati kwenye tukio na vitendo vya rushwa.
IGP afafanua
Akizungumzia dhana hiyo ya udhaifu, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema katika mkutano
huo walifanya tathimini kuhusu maeneo waliyofanya vizuri na yale
yasiyofanywa vizuri.
“Tumeona uwezo wetu kwenye utendaji, tumeandaa maazimio yatakayoeleza
namna nzuri ya kujipanga,” alisema Alisema sasa wanajipanga kuona hali
ya usalama inaimarishwa wakati nchi ikielekea kwenye Kura ya Maoni na
Uhaguzi Mkuu. “Utendaji mzuri ni ule wenye weledi na unaozingatia haki
za binadamu,” alisema.
Joseph Lugendo, Dar na Sifa Lubasi, Dodoma Via habarileo.