WAKURUGENZI
21 katika Halmashauri mbalimbali nchini wamevuliwa madaraka katika
kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015 huku 27 wakipewa onyo na sasa kesi zao
zikiwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo matumizi mabaya ya
fedha.
Aidha, wafanyakazi 233 wamefukuzwa kazi na mabaraza ya madiwani na
wengine 372 kesi ziko mahakamani huku 10 zikiwa zimetolewa uamuzi wa
kufungwa na wengine kutozwa faini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema
hayo wakati akijibu hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu madai ya kuhamisha watumishi wenye
tuhuma bila kuwachukulia hatua.
Ghasia alisema iwapo kuna watumishi waliohamishwa bila kujua na
inapofahamika wanarudishwa kituo cha kazi kujibu tuhuma kwani si sera ya
wizara yake kuwahamisha kwa makusudi watumishi wanaotuhumiwa kwa makosa
mbalimbali wanawachukulia hatua za kisheria.
Akizungumzia suala la miradi ya chini ya kiwango, alisema kuanzia
mwaka jana wamepitia muundo wao na kuunda idara ya ufuatiliaji na
tathmini ya ubora katika miradi ya halmashauri na ikiwa chini ya kiwango
hatua zinachukuliwa kabla Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
hajafika kukagua.
Katika suala la kuongeza mapato katika halmashauri, alisema mwaka
2013 walifanya utafiti wa kuainisha vyanzo vipya vya mapato na kupata
ushuru wa minara ya simu, nyumba za kulala wageni na halmashauri kutoza
kodi yamajengo.
“Lakini pia tunatarajia kurekebisha sheria ya fedha katika serikali
za mitaa na tayari rasimu ya kwanza imekamilika kwa lengo la kuongeza
vyanzo vya mapato katika halmashauri,” alisema.