Kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamevamia na kuvunja stoo ya Kituo kidogo cha Polisi Mngeta, Kilombero na kuiba bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 30.
Majambazi hao pia wanadaiwa kuiba jenereta, redio, viti, betri ya gari na spika ya redio.
Akizunguzia
tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul
alisema uporaji huo ulitokea usiku wa Februari Mosi.
Kituo
hicho ni cha tatu kuvamiwa mwaka huu baada ya Kituo Kikuu cha Polisi
Rufiji, Mkoa wa Pwani na Bukombe kuvamiwa na majambazi na kuua polisi
wawili na kupora bunduki saba na risasi 60.
Mwaka jana
majambazi walivamia Kituo cha Polisi Mkamba, wilayani Mkuranga, Pwani na
kuua askari mmoja na mgambo wawili kisha kupora bunduki tano na risasi
60.
Kadhalika, Juni mwaka jana, majambazi yalivamia
Kituo cha Polisi Bukombe na kuua askari wawili na kupora bunduki 10 na
risasi kadhaa.
Akizungumzia uvamizi huo, Kamanda Paulo alisema baada ya wizi
huo askari walianza msako na kufanikiwa kuipata bunduki hiyo na risasi
30, viti vitatu, jenereta na redio vikiwa vimefichwa katika pori la
Simbangingile lililopo Mngeta Wilaya ya Kilombero.
Polisi
inawashikilia watu watatu kutokana na tukio hilo ambao ni Ramadhani
Shewele (20), Hamisi Ahmed (45) na Ignus Shewele (34) wote wakazi wa
Nakagulu.
Alisema mtuhumiwa mmoja aliyetajwa kwa jina la Emmanuel Shewele (41) bado anatafutwa na polisi.
Kamanda Paul aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano ili kuwapata watuhumiwa wengine.