Huu ni ukatili namba moja kwa wanandoa duniani! Bado picha haijatoka kichwani kwa wakazi wa Manzese jijini Dar kufuatia kifo cha kuchinjwa cha Josephine Ndengaleo Mushi kinachodaiwa kufanywa na mume wake wa ndoa, Remy Joseph (35).
Tukio
hilo la kutisha kusimuliwa achilia mbali kuona, lilijiri saa 9: 10
alasiri ya Januari 29, mwaka huu ndani ya chumba kimoja kilichopo
ghorofa ya pili ya Hotel Friend’s Corner Ltd iliyopo Manzese Argentina,
Dar.
Baada ya habari za mauji hayo kusambaa kama moto wa kifuu, waandishi wetu walianza kuichimba habari hii kwa kina.
Kwa
mujibu wa mhudumu mmoja wa hoteli hiyo, Januari 28, mwaka huu, Remy na
Josephine walifika kwenye hoteli hiyo na kuchukua chumba. Walionekana
wenye amani, kwani hakuna sura iliyoonesha kuna tatizo.
“Walikuwa
kama wateja wengine. Tena niliwauliza kama wanatoka mkoa, wakasema ni
wakazi wa Dar es Salaam, wao ni mke na mume kwa ndoa, waliamua kulala
hapa ili kuimarisha mapenzi yao, si lazima kila siku nyumbani,” alisema mhudumu mmoja.
Kwa
mujibu wa baadhi ya wahudumu wa hoteli hiyo, siku ya pili, muda wa saa
tisa alasiri, walishtuka kuona damu nyingi ikitoka ndani ya chumba
walichopanga wawili hao.
“Tulishtuka
sana. Tukajua kuna kitu kikubwa kimewapata. Ilibidi tuwagongee mlango
ili tujue kilichowapata lakini mlango haukufunguliwa,” alisema mhudumu mwingine.
Kwa
vile ukimya ulitawala ndani ya chumba hicho huku damu zikiendelea
kutiririka, ilibidi uongozi wa hoteli hiyo yenye sifa ya ulinzi,
uwasiliane na Kituo cha Polisi cha Ndugumbi ambacho kipo jirani.
Polisi
walifika, wakagonga mlango kwa muda mrefu bila kufunguliwa mpaka
baadaye sana ambapo mlango huo ulifunguliwa na mwanaume akiwa ameshika
kisu mkono wake wa kuume.
Ndani
ya chumba kulionekana damu zimetapakaa kila sehemu. Polisi walimsihi
mwanaume huyo kuangusha kisu chini ili waongee lakini jamaa aligoma.
“Polisi
walimwamuru mwanaume atupe kisu chini, akakataa. Sura yake wakati huo
ilikosa mwonekano wa ubinadamu. Ndipo askari mmoja alitumia mbinu ya
kivita, alimpiga mkono wake wa kulia kwa kumshutikiza kisu kikaangukia
mbali, akawekwa chini ya ulinzi. Kumbe kile kisu mbali na kumuua mkewe
alikitumia kujaribu kujichinja koo lakini ikashindikana,” alisema mhudumu huyo.
Mwanaume
akiwa chini ya ulinzi na pingu mikononi, polisi waliingia chumbani na
kukuta damu kila mahali. Cha kusikitisha zaidi, mwili wa marehemu
Josephine ulipigishwa magoti, sehemu ya miguu mpaka magoti ikiwa
sakafuni na kifuani kulalia kitanda.
Halafu ulifunikwa shuka.“Kwa mbali ungeweza kusema kuna binadamu anasali kwa namna ambavyo marehemu huyo alivyokuwa amepigishwa magoti,” alisema mhudumu huyo.
Katika
hali iliyoonesha kuwa, mtuhumiwa baada ya kutenda ukatili huo alitaka
kujinyonga, polisi walikuta waya wa umeme wa tivii ukining’inia kwenye
pangaboi lakini ukiwa umekatika.
Polisi
walifanya uchunguzi chumbani na kugundua kuwa, marehemu Josephine
alichinjwa shingoni, akakatwa mbavu mbili, moyo na maini vilikuwa nje
‘vikimwagika’, mwisho alichomwa kisu utosini.
Pia
kwenye chumba hicho, polisi walikuta simu mbili, ya marehemu na ya
mtuhumiwa zikiwa zimeharibiwa laini kiasi cha kukosa mawasiliano.
Mwandishi
alipata bahati ya kuzungumza na mtuhumiwa huyo kabla ya kupelekwa Kituo
cha Polisi Magomeni, Dar ambapo alisema Josephine alikuwa mke wake na
wameishi kwa muda zaidi ya miaka kumi na kupata watoto wawili. Hata
hivyo, hakuongea zaidi ya hapo.
Msimamizi mkuu wa hoteli hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Zuberi Hussein alipohojiwa alisema:
“Tuliwapokea
hawa watu kama wateja wengine. Walilipa shilingi elfu kumi na tano kwa
chumba. Hatukujua kama haya yangetokea, wahudumu ndiyo walibaini baada
ya kuona damu ikitiririka mlangoni.”
Baadaye,
polisi waliupakiza mwili wa marehemu kwenye gari kuupeleka Hospitali ya
Taifa Muhimbili huku mtuhumiwa akipelekwa Kituo cha Polisi Magomeni
jijini Dar pembeni yake akiwa amelala marehemu mkewe.
Baada
ya hapo,Mwandishi wetu alifunga safari hadi eneo la Studio, Kinondoni,
Dar nyumbani kwa David Ndeshao Mushi ambaye ni kaka wa marehemu na ndiko
sehemu ulipowekwa msiba.
Baadhi ya ndugu wa marehemu walidai kwamba, Josephine na mumewe mara kwa mara walikuwa na migogoro ya ndoa.
“Ndoa
yao haikutulia, walikuwa wanapatanishwa lakini baada ya muda mfupi
wanaanza tena ugomvi. Mumewe alikuwa akimhisi vibaya mke wake. Hata
hivyo, Desemba mwaka jana, Josephine alienda kuishi kwa kaka yake
kutokana na ugomvi,”alisema mmoja wa wanandugu wa karibu.
Kaka mtu huyo alipohojiwa alisema: “Marehemu
alirudi kwangu lakini tulikuwa hatujaongea naye kuhusu ugomvi wao.
Nilisafiri mkoani nikamuacha, niliporudi, Jumatano alienda kazini lakini
hakurudi. Tulipopiga simu yake akawa hapatikani. Mumewe naye akawa
hapatikani hadi taarifa ilipotufikia kwamba kauawa hotelini.
“Tunatarajia
kusafirisha mwili kwenda Moshi, Jumapili (juzi). Mazishi yatakuwa
Jumatatu (jana). Marehemu ameacha watoto wawili ambao walikuwa wakiishi
Tabata, Dar.”
Inadaiwa
kuwa, mtuhumiwa alikuwa mfanyakazi wa Baa ya Break Point iliyopo jijini
Dar. Marehemu alikuwa mfanyakazi katika Kampuni ya TAC iliyopo Upanga,
Dar.
Mmoja
wa marafiki zake wa karibu alisema Jumatano mchana, mumewe alimfuata
kazini na wakawa na mazungumzo, alimtaka waondoke lakini marehemu
alikataa.Alimbembeleza sana mwishowe wakakubaliana na kuondoka lakini
wakashangaa kusikia alimuua hotelini.