WANACHAMA 13 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaotaka ubunge katika jimbo la Iringa Mjini wanaendelea kujinadi kwa wanachama wa chama hicho kwa kushindanisha mikakati yao ya kulikomboa jimbo hilo na kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Kwa miaka mitano iliyopita jimbo hilo limeongozwa na Mchungaji Peter Msigwa aliyechaguliwa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mbali na kuwashirikisha wanachama wake wote, kampeni hizo ambazo tayari zimefanyika katika matawi ya kata za Nduli na Kihesa zimewavutia pia wafuasi wa baadhi ya wagombea hao.
Pamoja na kuwavuta wafuasi wa wagombea hao, Katibu wa CCM wa Manispaa ya Iringa, Elisha Mwampashi amewaambia wanachama hao kwamba:
“Chama kinahitaji mgombea mwenye hadhi ya kurejesha jimbo hili mikononi mwa CCM, anayetokana kwa njia ya haki na wana CCM wenyewe na atakayekubalika na watu wote.”
Mwampashi aliwataka wanachama hao kuwapima wagombea hao kwa hoja na mikakati yao ili wapate mgombea safi atakayekivusha chama hicho salama.
Balozi Dk Augustino Maiga
Katika mikutano iliyofanyika katika kata hizo, Dk Maiga aliyekuwa mmoja kati ya wagombea 38 waliokuwa wakitafuta ridhaa ya chama hicho kuwania urais alisema atatumia uwezo na ujuzi wa kiuongozi na kidiplomasia aliopata ndani na nje ya nchi kurudisha heshima ya CCM katika jimbo la Iringa Mjini kwa kulikomboa kwa kutumia mikakati na mawazo mapya.
“Pili nitaleta mambo mapya yatakayofanana na mahitaji ya sasa ya jimbo letu katika sekta mbalimbali kama afya, elimu, miundombinu, biashara, kilimo, ujasiriamali” alisema.
Ili yote hayo yaweze kufanikiwa, Dk Maiga aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuisadia nchi ya Somalia iliyosambaratika kwa zaidi ya miaka 25 kupata katiba, bunge na serikali:
Alisema hayo yote yatafanikiwa kwasababu atatumia mawazo na mbinu mbadala ambazo ni mchanganyiko maalumu wa uongozi wa kimataifa atakaoutafsiri katika ngazi ya kitaifa na kijimbo.
Dk Yahaya Msigwa
Mgombea huyo ambaye pia ni Katibu wa Siasa, Uenezi na Itikadi wa CCM Mkoa wa Iringa alisema; “nina uwezo wa kuing’oa Chadema katika jimbo hili.
Dk Msigwa alisema atahakikisha manispaa ya Iringa inapata hadhi ya jiji, vyuo vikuu vilivyopo vinawanufaisha wakazi wake, huduma za afya zinaboreshwa na matumizi ya yanakuwa endelevu kwa manufaa ya wahusika wenyewe.
Mahamudu Madenge
Mgombea huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema kazi ya kuiong’oa Chadema katika jimbo hilo alianza kuifanya muda mrefu.
“Kama MNEC nilianza kwa kufanya semina kwa mabozi na wanachama wote wa jimbo la Iringa ili wajue wajibu na majukumu yao katika kukitetea chama chao,” alisema.
Akizungumzia maendeleo katika jimbo hilo alisema atahakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa ipasavyo katika ngazi ya jimbo hilo.
Aidan Kiponda
Alisema; “ndoto yangu ni kuufanya mji wa Iringa uwe wa kibiashara. Nitahakikisha wananchi wanapata elimu ya ujasiriamali ili wajiajiri wenyewe.”
Kiponda alisema atawashawishi wafanyabiashara wenzake ili wajenge au kuanzisha viwanda vya kutosha ili vitoe ajira.
Frank Kibiki
“Naomba kazi ya kuwa mtumishi wa wana Iringa, siombi kazi ya kununua utumishi wa wana Iringa,” alisema Kibiki ambaye ni mwandishi wa habari wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo wa mjini Iringa.
Alisema CCM inahitaji mgombea anayeweza kuunganisha chama, asiye na dosari, mwenye maono na mwadilifu, sifa ambazo anazo.
Alisema CCM inaweza kuishinda changamoto ya kushinda dhidi ya upinzani kwa kuwa na mgombea wa kawaida anayezijua changamoto kwa kuangalia mahitaji ya wanachama na wapiga kura ndani na nje ya chama
Alisema endapo azma yake hiyo itafanikiwa changamoto zinazogusa vijana, wazee, akina mama, walemavu na watoto atazifanya ajenda yake ya kudumu kwani zinahitaji utatuzi wa kweli na mikakati ya dhati.
Frederick Mwakalebela
Mgombea huyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe alisema; “mwaka 2010 mlinipa ushindi wa kishindo katika kura zetu za maoni, yakajitokeza mambo na kufanya safari yetu isifike mwisho; nimerudi tena nikiwaomba imani ile ile.”
Alisema upinzani una hofu kubwa endapo atapewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho kwa kuwa rekodi yake katika masuala ya kimaendeleo inafahamika.
Addo Mwasongwe
“Mimi ni mtu ninayemuamini Mungu, ninachukia rushwa na ninayependa maendeleo. Nipeni kura yenu ili Chadema wawape heshima yenu ya kuchagua mtu makini wa kupambana nayo,” alisema.
Alisema endapo atapata ridhaa hiyo vipaumbele vyake vitakuwa katika sekta zote ikiwemo sekta ya elimu, afya, kilimo, ardhi, maji na miundombinu.
Jesca Msambatavangu
Alisema yeye ni mpambanaji mwenye uwezo wa kukatiza pia kwenye njia zinazotumiwa na wafuasi wa Chadeama anayejua namna kuking’oa chama hicho.
Kuhusu maendeleo alisema; “siongelei kuhusu kuanza kufanya, mnajua mimi ni mtu wa kujitolea katika maendeleo ya watu, nimeanza kufanya hivyo muda mrefu na nitaendelea kufanya hivyo nitakapopewa au kutopewa ridhaa ya kuwa mbunge.”
Michael Mlowe
“Tusiwe mashabiki wa kupiga makelele bila kuangalia uhalisia wa mambo, kuna watu walitusaliti tukapoteza ubunge 2010, tujifunze kupitia alama za nyakati kama tunataka kukomboa jimbo hili,” alisema.
Alisema wapo watu wanaokigawa chama mchana kweupe lakini ndio wanaoshabikiwa kwa kupelekwapelekwa na madalali wa siasa.
Alisema anayo mengi ya kulifanyia jimbo hilo katika sekta mbalimbali za maendeleo endapo atapewa ridhaa hiyo.
Nuru Hepautwa
Mgombea huyu alisema; “mimi ndio chaguo sahihi la kupambana na upinzania Iringa Mjini.”
Alisema endapo atapata ridhaa hiyo, atahakikisha anafuatilia na kudhibiti matumizi mabaya ya mapato ya halmashauri ya manispaa ya Iringa ili yatumike kwa maendeleo ya jimbo.
“Kuna fedha nyingi zinatakiwa kutolewa kwa ajili ya vijana na wanawake lakini haifanyiki hivyo. Nitahakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa ili ziwasaidie kubadili maisha yao,” alisema.
Fales Kibasa
“Vijana na akina mama ndio wanaoongoza nguvu ya uchumi katika eneo husika kwahiyo lazima wapate ajira,” alisema.
Alisema atahakikisha anawatumia vijana hao ili waipatie Chama cha Mapinduzi ushindi dhidi ya vyama vya upinzani.
Mbali na ajira alisema atahakikisha huduma za afya zinatolewa, huduma ya maji inapatikana kwa kiwango kinachotakiwa, elimu inakuwa fursa ya jirani kwa wote na miundombinu ya barabara inaboreshwa.
Peter Mwanilwa
“Napenda mimi niwe mgombea kupitia chama hiki lakini endapo sitapata fursa hiyo nitamuunga mkono atakayechaguliwa kupeperusha bendera yetu,” alisema.
Mwanilwa ambaye pia ni Afisa Tarafa mkoani Dodoma alisema endapo atapewa ridhaa hiyo atahakikisha shughuli za kijasiriamali zinaboreshwa ili kubadili maisha ya watu wake.
Kampeni hizo zitakazofuatiwa na kura za maoni za chama hicho zitakazofanyika Julai 31, mwaka huu zitaendelea kesho katika kata ya Mkwawa.