ASKARI wa Jeshi la Polisi amejeruhiwa na madereva wa pikipiki maarufu
kama bodaboda katika fujo zilizoibuka juzi jioni katika eneo la Mzinga,
Kongowe Mbagala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam katika Manispaa ya
Temeke.
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo jana, Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Temeke, Kihenye Kihenya alisema askari walikuwa
kwenye doria kwa kutumia pikipiki maarufu kama Tigo na walipofika eneo
la Mzinga walimkamata dereva mmoja aliyebainika kuwa na matatizo kadhaa
kwenye pikipiki yake.
“Polisi walimkamata mwendesha pikipiki mmoja na ikabainika kwamba
alikuwa na makosa kadhaa ambayo yalimpasa alipe faini. Lakini madereva
wenzake walipoona amekamatwa wakaanzisha fujo na kumjeruhi mmoja wa
askari kwa kumpiga chupa usoni,” alisema Kihenya.
Aliongeza kuwa “Tumekamata bodaboda kumi na tano na tayari
tunaendelea na uchunguzi ili kuweza kubaini wahusika wakuu na tuweze
kuwafikisha mahakamani kwa kosa la shambulio,” alieleza.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema fujo hizo zilikuwa kubwa kiasi
kwamba polisi walilazimika kuwatawanya washambuliaji kwa kupiga risasi
za moto hewani.
“Mimi nilifunga duka nikakimbia maana kulikuwa hakukaliki hapa,
walipompiga yule askari, uso wote ulitapakaa damu ndipo wakarusha risasi
hewani. Kila mtu alikimbilia anakojua mwenyewe,” alisema moja wa
mashuhuda aliyeogopa kutajwa jina lake.
Kwa upande wake, Sanja Justin, alisema yeye alikuwa ana safari ya
kwenda Mbagala na alipokaribia kituoni cha basi, alisikia mlio wa risasi
na kuamua kukimbia na kurudi nyumbani.
“Nilitaka kwenda kupanda gari nielekee Mbagala lakini nilipofika
karibu na kituo nikasikia mlio wa risasi, nikarudi mbio na kila mtu
alikuwa kwenye harakati za kukimbia ili kujiokoa na matatizo,” alisema.
Eneo la Mziga limekuwa na matukio mengi ya kihalifu ambapo mwishoni
mwa mwaka jana kuliibuka kikundi cha kihalifu kilichojiita Black Amerika
na kusababisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
Hata hivyo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kulidhibiti kundi hilo na kurejesha hali ya utulivu kwa wakazi wa eneo hilo.