TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), jana
iliwapandisha mahakamani Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu na
wakurugenzi wawili kwa makosa mawili yanayohusiana na rushwa kinyume na
Kifungu cha 32 cha Sheria ya Takukuru Namba 11 ya mwaka 2007.
Katika kesi hiyo inayowaunganisha maofisa wengine wawili wa
halmashauri ya wilaya ya Mufindi, wanatuhumiwa kuisababishia halmashauri
hasara ya Sh milioni 3.
Kesi hiyo iliyopewa jina la kesi ya uhujumu uchumi namba moja ya
mwaka 2015, ilifunguliwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Mufindi
mkoani hapa.
Mkuu wa wilaya hiyo na watuhumiwa hao wengine kwa pamoja wamekana
mashitaka yao mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Victoria
Nongwa.
Watuhumiwa wengine katika shitaka hilo ni Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Mikindani mkoani Mtwara, Limbakisye Shimwela ambaye wakati
kosa hilo likitendeka kati ya Desemba 2010 na Februari 2011, alikuwa
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi na mwingine ni Mkurugenzi
wa halmashauri ya Biharamulo mkoani Kagera, Nasibu Bakari.
Watuhumiwa wengine waliofikishwa katika mahakama hiyo, kutokana na
ushiriki wao wa makosa katika kesi hiyo ni Ofisa Mipango wa Halmashauri
ya Mufindi, Cosmas Mduda na Fundi Ujenzi wa wilaya hiyo, Fedrick Zaveri.
Akisoma shitaka linalowakabili watuhumiwa hao mahakamani hapo,
Mwendesha mashitaka wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Imani Mizizi alidai
mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo kuwa kati ya Desemba 2010 na
Februari 2011 watuhumiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa
la rushwa kinyume na kifungu cha 32 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na
rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Katika kosa la pili, linalowakabili watuhumiwa watatu katika kesi
hiyo, ambao ni Shimwela ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Mtwara/Mikindani, Bakari ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Biharamulo na Cosmas ambaye ni fundi ujenzi, ni lile la matumizi
mabaya ya ofisi kinyume na kifungu cha 31 cha sheria kuzuia na Kupambana
na Rushwa.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya Desemba 2010 na Februari 2011,
watuhumiwa hao watatu walitumia ofisi vibaya kwa kuingia mkataba na
Fedrick Zaveri kwa ajili ya ujenzi wa vyoo, bafu za kuogea na mfumo wa
maji katika shule ya sekondari ya Ihalimba bila kufuata Sheria ya
Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.
Ilidaiwa kuwa kutokana na ha Watuhumiwa wote wamekana kosa na
kuachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya kila mmoja kuwa na
wadhamini wawili na bondi ya Sh milioni moja kwa kila mdhamini.
Hakimu Victoria aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 13 mwaka huu, watu hao watakapokuja kusomewa maelezo ya awali.