WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameagiza watendaji katika Manispaa na Jiji
waliohusika kunyang’anya mali za wafanyabiashara mbalimbali kwa
kisingizio cha kusafisha jiji na kugawana badala ya kupeleka
kunakoruhusiwa kuchukuliwa hatua huku akiahidi kumshughulikia Katibu
Tarafa wa Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Aidha, amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kukaa na wafanyabiashara na
kuangalia njia nzuri ya kufanya biashara ili kuondoa vurugu baina yao
na vijana.
Pinda aliyasema hayo jana wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa
hapo kwa Waziri Mkuu alipojibu swali la Mbunge wa Ilala, Iddi Zungu
(CCM) aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu wanamgambo wanaotumia
nafasi ya kusafisha jiji kuwanyanyasa wafanyabiashara na kugawana mali
zao huku tatizo kubwa likiwa kwa Katibu Tarafa wa Kariakoo.
Amesema yeye binafsi alitumiwa picha ya watendaji hao wakigawana mali
walizowanyang’anya wafanyabiashara wakiwamo mama lishe, jambo ambalo ni
kuwanyanyasa na kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
Waziri Mkuu alikemea kitendo cha watendaji wa jiji na mikoa kutumia kusafisha jiji kunyanyasa wananchi.
Hivyo aliagiza wakuu wa wilaya na mikoa kukaa na wafanyabiashara
ndogo na kupanga jinsi ya kuendesha biashara kistaarabu ikiwa ni pamoja
na kupanga masoko ya jioni na Jumapili ili wafanye biashara muda mfupi
na kuondoka.