CUF yaapa kuendelea na maandamano kila mwaka


Chama cha Wananchi (CUF) kimesema, hakitarudi nyuma na kitaendelea kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kila Januari 26 na 27 kila mwaka kuazimisha mauaji ya wanachama wake yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001. 
 
Katika maadhimisho yaliyofanyika mwaka huu, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama 32 wa chama hicho walipigwa kisha kushikiriwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kuendesha maandamano yasiyokuwa na kibali.
 
Kutokana na kosa hilo, jana Profesa Lipumba alipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar na kusomewa shitaka la kuhamasisha wafuasi wa chama hicho kutenda kosa la jinai.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo, Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Juma Duni Haji alisema hakuna ubaya wowote kuwaenzi na kuwakumbuka wapendwa wao kwa kufanya mikutano na maandamano.
 
“Jeshi la Polisi linatakiwa kutambua ya kwamba kila Januari 26 na 27 tutaendelea kufanya mikutano na maandamano, kama hawataki kuelewa hilo wakae mkao wa mapambano na wananchi kila mwaka.
 
 “Nadhani maadhimisho ya Januari 26 na 27 mwaka 2016 yatakuwa makubwa zaidi kulingana na Jeshi la Polisi litakavyokabiliana nayo,” alisema Haji
 
Aliongeza: “Jeshi la Polisi limekosa maadili halifai, linahitaji marekebisho makubwa na tunamtaka Rais (Jakaya Kikwete) kuwawajibisha wahusika wote wa tukio hili-viongozi wa Jeshi la Polisi.”
 
Haji alisema, “Tunalaani kupigwa kwa viongozi na wafuasi wa Chama chetu na Jeshi la Polisi na tunalitaka kutekeleza majukumu yake kwa kutumia weledi na kuacha ushabiki na kutumiwa kisiasa kwa visingizio vya kiitelinjensia.”
 
Kuhusu afya ya Profesa Lipumba, Mkurugenzi wa Fedha wa CUF, Joran Bashange alisema, “Profesa Lipumba Manaendelea vizuri na kwa ushauri wa daktari amemwambia apumzike kwa siku tatu bila kufanya kazi ya aina yoyote.”
 
Aliongeza: “Mwenyekiti (Lipumba) hana maradhi ya shinikizo la damu lakini kutokana na kadhia hiyo ndiyo iliyosababisha yeye kupata shinikizo hilo kwani alipokamatwa alitumia saa 6 kuhojiwa na polisi waliokuwa wakibadilishana mahojiano yaliyofikia hatamu saa 6 usiku.”


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo