BUNGE jana lilivurugika na kulazimu Spika Anne Makinda kuliahirisha
hadi leo, kutokana na wabunge wa upinzani kushinikiza ijadiliwe hoja
kuhusu kupigwa kwa wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) katika vurugu
zilizotokea juzi wilayani Temeke, Dar es Salaam.
Awali Makinda baada ya kutokea kwa vurugu hizo, alikuwa ameahirisha
Bunge hilo hadi jana jioni, lakini baadaye alilazimika kuahirisha
shughuli zote za Bunge hadi leo baada ya kamati ya uongozi kukutana na
kukubaliana shughuli za jana zisitishwe.
Alisema baada ya kamati ya uongozi kukutana kwa muda mrefu, ilikubaliwa kwamba suala hilo lipelekwe kwenye kamati ya kanuni.
Chanzo cha vurugu
Kwa mujibu wa gazeti la habari leo ni kwamba Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) ndiye aliyewasilisha
hoja jana bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu kwa kuzingatia
Kanuni ya 47, akitaka Bunge liahirishe shughuli zake, wabunge wajadili
suala hilo.
Spika Makinda alikubaliana na hoja ya suala hilo kujadiliwa bungeni;
lakini kwa kuiagiza Serikali itoe kauli leo na baada ya hapo, wabunge
wajadili.
“Kwa mazingira haya naiagiza serikali kesho (leo) itoe kauli kamili
ambayo sisi tutaelewana, halafu mimi kesho naruhusu mjadala siyo leo
(jana),” alisema Spika.
Baada ya maelezo hayo, spika alitoa nafasi kwa Katibu wa Bunge,
kuendelea na shughuli ambazo kwa mujibu wa ratiba, Mwenyekiti wa Kamati
ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto, alipaswa kuwasilisha taarifa
ya Kamati za Hesabu za Serikali za Mitaa, maoni na mapendekezo yaliyomo.
Hata hivyo, wabunge hao wa upinzani waligomea uamuzi huo wa spika.
Baadhi yao walisimama na kuanza kurushia kiti cha spika maneno, kuonesha
kutokubali mjadala huo kufanyika leo.
“Haya nendeni kama mnataka, muwe na busara. Hatuwezi kuanza
kutukanana hapa…waheshimiwa, kama mnataka kufanya mnachofanya fanyeni.
Wote ni watu wazima tutumie busara. Mnachotaka kufanya fanyeni, lakini
hamtumii busara. “Mheshimiwa Mbatia amesema vizuri, suala hili linataka
amani na mshikamano…” alisema Makinda na kumuita Mwenyekiti wa PAC,
awasilishe taarifa ya kamati, lakini haikuwa hivyo kutokana na wabunge
kuendelea kusimama na kupiga kelele.
“Mnafikiri huu ni mtindo wa kanuni? Huu si mtindo wa kanuni... naomba
mkae chini,” alisema bila kusikilizwa na wabunge hao, hali iliyomlazimu
Makinda kuketi zaidi ya dakika kadhaa, kutoa nafasi kwa wabunge hao
kukaa, jambo ambalo halikufanyika. Badala yake, waliendelea kupiga
kelele na kurushia kiti maneno.
Baadaye, Spika alisimama tena na kuwaambia, “Tatizo mlilo nalo ninyi
ni dogo sana. Jambo hili ni kubwa sana…ninachosema jambo hili ni kubwa
sana. Na kama ni kubwa sana, hamuwezi kuzungumza kama mnavyozungumza
sasa. “Ni vizuri watu wote wakaelewa. Na mtoa hoja, Mbatia tumezungumza
akiwepo Tundu Lissu, akiwemo Injinia Mnyaa (Habib) na ndiyo mimi
niliwaruhusu kwamba, hili suala Mbatia atasema halafu naitaka serikali,
nimesema kesho…,” alisema na kukatishwa kelele za wabunge hao,
wakishinikiza mjadala uwe jana, jambo ambalo Spika aliamua kuahirisha
shughuli za bunge hadi jioni.
Hoja za Mbatia
Awali katika kuwasilisha hoja yake, Mbatia ambaye alikiri kwamba
yeye, Mnyaa na Lissu walikutana na Spika Makinda na kukubaliana juu ya
suala hilo, alitumia Kanuni ya 47 inayoruhusu jambo la dharura lenye
maslahi kwa umma lijadiliwe bungeni.
Alisema wanachama hao wa CUF, walifuata taratibu zote za maandamano
na kwamba hatua za mwisho waliyazuia na kwamba Profesa Lipumba alionesha
ushirikiano, lakini polisi wakaamua kutumia nguvu dhidi ya raia ambao
hawakufanya vurugu.
Alisema walimpiga Lipumba, waandishi wa habari walipigwa virungu na
wakati huo huo watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano walipigwa
mabomu.
“Jeshi la polisi, lilitoa kauli kwamba tuna maagizo kutoka juu… hili
ni jambo ambalo halikubaliki, ni jambo la kudhalilisha. Mwaka juzi
waandishi wa habari waliuawa, jeshi likawa linaua raia na raia wakaua
polisi, viongozi wa dini wakaingizwa huko kuuawa, jeshi la polisi
likaingizwa katika hali ya sintofahamu. Na sasa linaanza kujirudia tena
kwa kasi kubwa, kwa dharau kubwa na kudhalilishwa.
“Profesa Lipumba ni mwenyekiti wa chama chenye wabunge wengi humu
zaidi ya 35, ni mwenyekiti chama chake kinashiriki serikali ya umoja wa
kitaifa Zanzibar, mheshimiwa Lipumba kama anaweza kudhalilishwa kiasi
hicho, raia wengine wanaweza wakafanywa namna gani? alihoji Mbatia.
Kwa mujibu wa Mbatia, wabunge hao wanataka kufahamu agizo hilo la
kupigwa Lipumba na wanachama wake limetoka kwa nani, kwa maslahi gani.
Alisema jambo hilo ni la kudhalilisha na la hatari ambalo halipaswi
kuachiwa liendelee, ikizingatiwa Julai mwaka juzi, vyama vilikaa na Rais
Jakaya Kikwete na kukubaliana juu ya masuala ya amani na utulivu wa
nchi.
Makubaliano na Spika
Akizungumza na waandishi nje ya ukumbi juu ya makubaliano yao
(Mbatia, Lissu na Mnyaa) ya awali na spika, Mbatia alikiri kwamba jana
asubuhi walimwendea spika na kuzungumza naye suala hilo, akawakubalia
kwamba ataitaka Serikali ijibu kisha ufanyike mjadala.
Hata hivyo, Mbatia alisisitiza kwamba serikali ilitakiwa iwahi kutoa
maelezo kabla ya wabunge kuingilia kati. Alisisitiza kwamba maelezo ya
awali, yalitakiwa yatolewe jana.
Mbatia aliendelea kushutumu Polisi, akisema inaitoa nchi kwenye
mstari wa amani, tofauti na makubaliano yaliyofanyika Julai mwaka juzi,
ambayo nchi ilirudishwa katika hali ya kawaida.
Awali, asubuhi kabla ya kuingia bungeni kwenye kipindi cha maswali na
majibu, wabunge wanaounda Ukawa walikutana katika ukumbi wa Msekwa na
kufanya kikao, ambacho hoja kuu ilikuwa ni juu ya vurugu hizo za CUF.
Wapinzani washutumiwa
Wakizungumzia hali hiyo ya vurugu bungeni, baadhi ya wabunge,
walishutumu upinzani kwa madai ya kutoheshimu kiti sanjari na kanuni za
Bunge.
Baadhi walisema kwa kuwa suala hilo lilikuwa jipya, hapakuwa na haja
ya kuharakisha kulijadili jana. Baadhi walidai hawakuwa na taarifa
kamili ya yaliyojiri kwenye maandamano hayo hivyo walihitaji
kujiridhisha kabla ya kuanza mjadala.
“Spika ameipa nafasi serikali itoe taarifa…tungeanza kujadili leo,
wabunge wangejadili nini? Haiwezekani tukashitukizwa,” alisema Mbunge wa
Nkenge, Asumpta Mshama (CCM) na kushutumu waliokaidi kutii amri ya
spika kuwa wanaendelea kudhalilisha Bunge.