TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inachunguza tukio la kupigwa kwa viongozi na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) katika tukio la jijini Dar es Salaam juzi, kubaini kama kulikuwa na matumizi ya nguvu ya ziada ya polisi dhidi ya raia.
Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe ambaye alisema pia ameagiza Idara ya Malalamiko ndani ya Wizara kufanya uchunguzi kuhusu matumizi ya nguvu za ziada, zichukuliwe hatua kwa watakaobainika kuhusika.
Waziri alikuwa akitoa taarifa bungeni, kabla ya wabunge kujadili hoja iliyowasilishwa juzi na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia akitaka ijadiliwe kuhusu kupigwa kwa wanachama wa CUF na matumizi ya nguvu ya ziada yaliyofanywa na polisi katika tukio hilo la wilayani Temeke, Dar es Salaam.
“Malalamiko haya ni mazito, na Serikali haiwezi kufumbia macho… pamoja na uchunguzi unaofanywa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, nimeagiza Idara ya Malalamiko ndani ya Wizara ifanye uchunguzi kuhusu matumizi ya nguvu za ziada na ikithibitika kwamba kuna polisi walitumia nguvu nyingi zaidi dhidi ya raia, basi tutachukua hatua mwafaka dhidi ya wahusika wote. Na hii ni ahadi,” alisema Chikawe.
Alisema Jeshi la Polisi halipaswi kutumia nguvu kuliko zinazohitajika katika kukamata wahalifu wa makosa ya jinai.
“Serikali inaomba radhi kwa wananchi wote waliokumbana na kadhia hii bila wao kujihusisha na kuwasihi wananchi kujiweka mbali na matukio yote ya uvunjifu wa sheria,” alisisitiza.
Alisema Serikali inaendelea kuahidi kuliongoza jeshi kwa kuzingatia sheria na maudhui yake sanjari na kukabili changamoto kuhakikisha kunakuwa na usalama na utulivu nchi nzima.
Hata hivyo, alisema Polisi haitaogopa wala kumwonea haya mtu yeyote bali itaendelea kutekeleza wajibu kwa kuzingatia haki za binadamu.
Kuzuiwa maandamano
Waziri Chikawe alieleza Bunge sababu za chama hicho cha siasa kuzuiwa kufanya maandamano na kusema ni baada ya Jeshi la Polisi kuona kwamba yanaweza kusababisha kuvunjika amani na kuathiri usalama wa taifa.
Kwa mujibu wa Waziri, Januari 26 mwaka huu Jeshi lilipokea barua kutoka CUF, ikitoa taarifa kuhusu kufanyika maandamano na mkutano wa hadhara Januari 27 kuadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya wafuasi wao yaliyotokea mwaka 2001.
Alisema baada ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupokea barua, iliwaita viongozi wa CUF kwa mazungumzo na kuwafahamisha matatizo yanayoweza kutokea.
Chikawe alisema matukio ya ugaidi hususani ulipuaji mabomu katika mikusanyiko kuwa ni miongoni mwa mambo ambayo yalihofiwa kwamba yanaweza kutokea kupitia maandamano hayo.
Alisema Polisi baada ya kupokea barua ya CUF, ilikutana na viongozi wao, ikawaeleza kwamba kufanya maandamano hayo yanayolenga kuadhimisha mauaji, pia kunaweza kusababisha chuki.
Pia ilielezwa kwamba taarifa za polisi zilionesha kunaweza kufanyika vurugu. Waziri Chikawe alieleza Bunge kwamba, kesho yake Polisi ilipata taarifa kuhusu kuwapo kwa mkusanyiko mkubwa wa watu kwenye ofisi za CUF wilaya ya Temeke.
Alisema Kaimu Kamanda, Sebastian Zakaria alikwenda na kukuta wanachama wapatao 200 wakiwa na mabango yenye maandishi mbalimbali ikiwemo, ‘Polisi na wanajeshi acheni kutumika na CCM,’; ‘tunaadhimisha kumbukumbu ya kuuawa kwa wenzetu, polisi acheni kutunyanyasa na kutumikia CCM kama vibaraka.’
Alisema Profesa Lipumba aliwasili katika ofisi hizo na alionekana kukaidi zuio na kuhamasisha wanachama kufanya maandamano kuelekea Mbagala Zakhem.
Kaimu Kamanda huyo baada ya kuona yakiendelea kinyume na zuio, alitangaza ilani ya kutawanyika, lakini waandamanaji walikaidi. “Ndipo akaamuru waandamanaji wakamatwe. Polisi wakatumia mabomu,” alisema Waziri.
Waziri alisisitiza kwamba polisi wanayo mamlaka kuzuia mkutano au maandamano, wakiridhika kwamba yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani. Alisema sheria inaruhusu mtu asiyeridhika na masharti na amri iliyotolewa, kukata rufaa kwa waziri, jambo ambalo viongozi wa CUF hawakufanya.
Mwanasheria Mkuu akwama
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju aligonga mwamba bungeni kuzuia mjadala huo kuhusu vurugu baada ya ushauri wake kutozingatiwa na badala yake, Spika Anne Makinda kuuruhusu.
Baada ya Waziri Chikawe kuwasilisha taarifa yake, Masaju alishauri Bunge lisijadili suala hilo kwa kuwa liko mahakamani. Lakini, Spika Anne Makinda alisema alipoamua mjadala ufanyike jana, hakulenga kwamba Serikali iende mahakamani.
Alisema sababu ya kusubiri suala hilo lijadiliwe jana, kwa kuwa watu walikuwa hawafahamu kinachoendelea. Aliruhusu mjadala kwa kutoa dakika tatu kwa kila mchangiaji, jambo ambalo pia lilipingwa na hivyo kulazimu atoe dakika 10.
Akihitimisha mjadala wa hoja aliyoiwasilisha bungeni juzi, Mbatia alishauri kuwepo tume ya kusimamia serikali vizuri kwa mujibu wa Katiba ili kuona namna ya kufanyia marekebisho sheria kadhaa, kusaidia Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla.
Mbatia alisema Bunge linahitaji kuangalia upya sheria ya vyama vya siasa, Sheria ya Haki na Kinga za Bunge Namba 3 ya 1988 na sheria ya Polisi.
“Na wote kwa pamoja tuombe Bunge lako aidha liwe na tume, ya kuisimamia serikali vizuri kwa mujibu wa Katiba ili kuweza kuona ni namna gani sheria hizi zifanyiwe marekebisho haraka ili uchaguzi mkuu ujao uwe na amani na utulivu na tulisaidie Jeshi la Polisi, tuisaidie serikali na nchi kwa pamoja,” alisema Mbatia.
Aliongeza kuwa, vipo vitendo vya kihuni ndani ya Jeshi la Polisi jambo ambalo alitaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu arejee kwa Saidi Mwema aliyestaafu wadhifa huo kushauriwa.
Mbunge huyo alimpongeza Spika Anne Makinda kwa busara zake za kuruhusu mjadala huo na kuonya wabunge kuacha kuingiza siasa katika suala hilo, kwani wakianza kurushiana maneno, hawatakuwa wanajenga taifa.
Awali katika mjadala, wakati baadhi ya wabunge walilenga kujadili suala hilo kwa misingi ya vyama vyao, Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF) alionya kulichukulia kivyama.
“Ushauri wangu kwa Bunge, kwa heshima na taadhima suala hili hata kama ni kweli kwamba CCM inasaidiwa, jambo hili tusilichukulie kivyama. Najua wabunge wengine wa CCM wameshaumizwa na Jeshi hili la Polisi,” alisema Mnyaa.
Alishutumu kwamba mbali ya kutumia nguvu, polisi ilitumia silaha zisizowajibika kutumiwa na jeshi, ikiwemo matumizi ya spana ya kutolea tairi kupiga watu vichwani.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) alishutumu Jeshi la Polisi akisema wapinzani wanapigwa na polisi, si kwa sababu wana makosa, bali wapo mafashisti ndani ya jeshi hilo na serikalini.
Alisema viongozi wote wa vyama vya siasa, hakuna asiyekuwa na majeraha ya Jeshi la Polisi na hakuna ambaye hajawahi kukamatwa na kunyanyaswa.
“Tuunde tume au kamati teule kuchunguza mauaji yote, polisi kujeruhi kupiga watu ili tupate ufumbuzi wa kudumu wa hili suala,” alisema Lissu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema kinachoendelea katika jeshi hilo, kimekwishafanyiwa uchambuzi na Jumuiya ya Madola kwamba lina mifumo ya kikoloni, ambayo lengo lake ilikuwa ni kuhakikisha wakoloni wanabaki madarakani na Waafrika hawaingii madarakani.