Hatimaye Abdulkarimu Thabiti Hasia aliyekuwa akituhumiwa kwa ugaidi, amefariki katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru alipokuwa amelazwa kwa miezi sita akiwa mikononi wa polisi.
Taarifa
ya kifo cha Hasia aliyekuwa mmoja wa maimamu wa Msikiti wa Geti la Mbao
Mbauda, ilitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Arusha
wakati kesi ya mtuhumiwa huyo na wenzake saba ilipotajwa.
Hasia
aliyekuwa ni mshtakiwa wa pili katika kesi ya kushambulia baa maarufu
ya Arusha Naighty Park, alikuwa akikabiliwa na makosa 16 ya ugaidi,
amefariki bila kufikishwa mahakamani hata siku moja.
Ilielezwa
mahakamani hapo jana, mbele ya Hakimu Hawa Mguruta kuwa mtuhumiwa huyo
alifariki Desemba mosi, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount
Meru.
Hata hivyo, wakati taarifa hiyo ikitolewa,
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Augostino Komba alieleza kutokuwa na
taarifa hiyo, hivyo mahakama iliagiza kubadilishwa hati ya mashtaka.
Baadhi ya ndugu wa marehemu walieleza kwamba tangu alipokamatwa
na kupata kipigo katika mahojiano na polisi, Hisia alikuwa amelazwa hadi
kifo chake.
Kifo cha mtuhumiwa huyo kimekuja wakati
kuna malalamiko ya watuhumiwa wengine kupigwa na kujeruhiwa na polisi
katika mahojiano na bado wapo gerezani.
Septemba 4 mwaka huu, mtuhumiwa huyo alisomewa mashtaka 16 ya ugaidi akiwa amelazwa hospitalini baada ya kupata fahamu.
Kabla
ya kusomewa mashtaka hayo, marehemu alikuwa ameshalazwa hospitalini
hapo kwa takriban miezi minne na awali ilishindikana kusomewa mashtaka
kutokana na kutokuwa na fahamu.
Kesi ya watuhumiwa
wengine wa ugaidi inatarajiwa kutajwa tena Desemba 19 kutokana na
kutokamilika kwa upelelezi na watuhumiwa hao walirejeshwa rumande.
