Klabu ya Yanga na wawakilishi wa
michuano ya shirikisho ya Afrika imewatupia virago rasmi makocha
wabrazil Marcio Maximo na msaidizi wake, Leonardo Neiva kwa kile
kinachoelezwa kutofurahishwa na mwenendo wa timu katika ligi licha ya
kuwa na wachezaji wengi mastaa wa kigeni na kutumia mamilioni katika
kusajili wachezaji mahiri wa kigeni.
Yanga hivi karibuni
ilimsajili mrundi na mfungaji bora msumu uliopita, Hamis Tambwe kutoka
kwa mahasimu wao (Simba) akiungana na Mliberia, Kpah Sherman,
Wanyarwanda Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na Mbrazil Andrey Coutinho
kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni
Tayari uongozi wa
Yanga, katika kile kinachoonekana pesa si tatizo, chini ya Mwenyekiti
bilionea Yusuf Manji umemrudisha klabuni aliyekuwa kocha wa zamani,
Mholanzi Van de Pluijm, atakayesaidiwa na kocha mzalendo na mchezaji wa
zamani wa timu ya Taifa na klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa.
Katika
maelezo yake, Manji amewatakia kila la kheri wabrazil hao na kusema na
mungu akipenda wataendelea kushirikiana nao katika siku za usoni.
Tayari makocha hao wawili ,
Pluijm na Mkwasa wameshatambulishwa kwa wachezaji wa Yanga na habari za
uhakika kutoka klabu hapo zinasema baada ya kusaini mkataba wa mwaka
mmoja na nusu, Pluijm, aliyewahi kuipatia yanga mafanikio katika ligi
kuu, ana anza kibarua chake rasmi leo.
Hata hivyo, kuondoka kwa
Maximo, aliyewahi kuajiriwa na Serikali ya Tanzania kama kocha mkuu wa
timu ya taifa, Stars Stars katika miaka ya nyuma na kurudi nchini
kivingine kuongoza Yanga, kumegubikwa na sintofahamu huku kukiwa na
habari kuwa bado anavutana na uongozi juu ya mafao yake kwa kuvunjiwa
mkataba.
Maximo, aliiongoza Yanga katika mechi tisa ndani ya miezi
mitatu (akipoteza mechi mbili katika mechi saba) baada ya kupokelewa
kwa shangwe uwanja wa ndege alipowasili kuwafundisha mabingwa hao wa
zamani wa Tanzania.
Inasemekana kuondolewa kwake kunatokana na
kipigo cha mabao 2-0 Yanga ilichokipata baada ya kufungwa na watani wao
wa jadi, Simba katika mechi isiyo ya ligi (Nani Mtani Jembe) chini ya
kocha Mzambia Patrick Phiri.
