Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe
Zitto amesema baada ya kukamilisha shughuli ya ufisadi wa Akaunti ya
Tegeta Escrow ambayo Sh306 bilioni zilichotwa, kamati yake sasa
inaelekeza nguvu katika kashfa nyingine nne.
Zitto
alisema kamati yake itatumia mwezi huu na Januari kupitia ripoti nne
ambazo zina masilahi kwa Taifa, ikiwamo ya utoaji wa vibali vya kuagiza
na kuingiza sukari nchini.
Alisema ufisadi katika
utoaji wa vibali hivyo ni mkubwa kuliko sakata la escrow... “Hili
linagusa moja kwa moja maisha ya wananchi, wamiliki wa viwanda na
uzalishaji. Tayari tumewaita Bodi ya Sukari tujadiliane kwa kina kuhusu
suala hili,” alisema.
Mbali na suala la sukari,
alizitaja ripoti nyingine kuwa ni ya uchunguzi wa ubinafsishaji wa Benki
ya NBC, ripoti maalumu ya Bandari na mikataba ya gesi.
“Baada
ya kazi ya PAC, tunapumzika, kwani kama unavyojua kazi ilikuwa ngumu,
wiki mbili nilikuwa silali. Kwa kuwa tuna ratiba ya wiki mbili. Kwa
Desemba na Januari tutaanza kuzifanyia kazi,” alisema Zitto ambaye pia
ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema).
Wiki
iliyopita, Bunge lilijadili ripoti ya PAC kuhusu ufisadi katika Akaunti
ya Tegeta Escrow na kuhitimishwa kwa kuweka maazimio manane yakiwamo ya
kuitaka Serikali iwawajibishe baadhi ya mawaziri na watendaji wengine
wakuu huku likitaka pia uchunguzi uendelee kwa wote waliotuhumiwa
kupokea fedha hizo kwa njia moja au nyingine.
Kauli ya
Zitto inakuja wiki moja baada ya wamiliki wa viwanda vya sukari vya
Kagera, Mtibwa na Kilombero kutishia kuvifunga kutokana na kuviendesha
kwa hasara.
Wamiliki hao walisema watafunga viwanda
hivyo kutokana na Serikali kushindwa kuzuia uagizwaji wa sukari nchini
kinyume cha taratibu.
Mkurugenzi wa Viwanda vya Kagera
na Mtibwa, Seif Seif alisema uagizaji wa sukari kutoka nje unafanyika
kwa ushirikiano wa wafanyabiashara wakubwa na vigogo serikalini kinyume
cha makubaliano na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya viwanda.
“Tulikubaliana
kwamba Serikali iwe inaagiza tani 100,000 kutoka nje lakini sukari
inayoingizwa sokoni ni zaidi ya tani hizo. Sukari tunayozalisha katika
viwanda vyetu ipo na haina pa kwenda,” alisema Seif na kuongeza:
“Leo
ukipita katika maduka utakutana na sukari ya kila aina, wafanyabiashara
wanaoagiza wanawatumia vigogo serikalini kuingiza sukari wapendavyo,
tena bila kulipa kodi,” alisema Seif.
Kutokana na hali
hiyo, Seif alisema wamelazimika kupunguza wafanyakazi 2,000 na kubakiwa
na 5,000 katika Kiwanda cha Kagera, Kilombero imepunguza 3,000 na
wamebaki 6,000 huku Mtibwa ikiondoa wafanyakazi 3,000.
“Hali
ni mbaya, si kama Watanzania wanavyofikiri. Tukifunga kabisa Watanzania
wengi watakosa ajira kama ambavyo mnaona wengine wamekosa, hatuwezi
kuendelea kufanya biashara ya hasara ambayo Serikali inaihalalisha,”
alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Sukari
Kilombero, Balozi Ami Mpungwe alisema: “Hali ni mbaya, tunaona kuliko
kuendelea na hali hii ni bora tusimame kuzalisha sukari.
“Serikali
kama kweli ina dhamira ya kuvifufua na kuviendeleza viwanda vyetu vya
ndani ni lazima kuvilinda na kupiga marufuku uagizwaji holela wa sukari
kutoka nje.”