Bibi Mariam Abdallah, mwenye umrin wa miaka 60, mkazi wa Kijiji cha
Mnanila, ambaye anadaiwa kushushiwa kipigo nyumbani kwake na Askari wa
JWTZ,akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma, Maweni
kwa matibabu.
Akielezea mkasa huo Mariam Abdallah alisema kuwa
Novemba 23 mwaka huu, majira ya saa tatu usiku, watu wanne waliokuwa
wamevalia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walivamia
nyumbani kwake wakimtafuta mwanamke aliyejulikana kwa jina moja la
Editha, ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa
wanajeshi hao ambaye hakufahamika mara moja jina lake.
Inadaiwa
kuwa siku moja kabla, askari huyo wa JWTZ, alikuwa amegombana na mpenzi
wake huyo, ugomvi uliosababisha askari huyo kung’atwa kidoleni na mpenzi
wake ambaye baada ya kitendo hicho alimtoroka, ambapo siku iliyofuata
aliamua kumtafuta hadi kwa bibi Mariam anaedaiwa kuwa ndugu wa mwanamke
huyo.
Hata hivyo baada ya kufika nyumbani kwake bibi huyo
aliwajibu kuwa hakuwa anafahamu alipo mwanamke huyo, lakini cha
kushangaza mmoja wa askari jeshi hao alianza kumshushia kipigo mfululizo
kwa mateke na ngumi na kumjeruhi sehemu mbali mbali za mwili wake hasa
maeneo ya usoni na kumsababishia maumivu makali kiasi cha kulazwa
hospitali.
“Walikuwa wanajeshi wanne, ila hao wengine
hawakunigusa mmoja ndiye alinipiga nikiakimbilia jikoni lakini
alinifuata hadi jikoni,”alisema Mariam.
Ofisa
Muuguzi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kigoma, Maweni, Siyaleo
Shilambele, alisema majeruhi huyo ameumia sana sehemu za usoni kiasi
ambacho jicho lake moja lilikuwa likitoa usaha na hawezi kuona vizuri.
“Bado
tunaendelea na uchunguzi wa kumfanyia vipimo mbali mbali na kumpa
matibabu ya awali na pia tumempiga picha za X-ray kichwani ili kuona
mifupa ya usoni iliumia kiasi gani,”alisema ofisa muuguzi huyo.
Mamlaka
za polisi hazikuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo ambapo imeelezwa
kuwa wakuu wa kipolisi wa mkoa wa Kigoma, wako nchini Burundi kwenye
ziara ya ujirani mwema.