Katika hali isiyotegemewa askari mmoja wa jeshi la kujenga Taifa (JKT)
anayesadikika kuwa ni wa kambi ya Mafinga wilaya ya Mufindi mkoani
Iringa usiku wa jana amenusurika kuvuliwa nguo za jeshi hadharani baada
ya kukutwa amelewa chakari na kulala katika mfereji wa maji machafu eneo
la nje ya stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani mjini Iringa
Tukio hilo lilitokea muda wa saa 2 usiku baada ya wasamaria wema kumshusha askari huyo kutoka katika basi la Mgumba ambalo alikuwa amepanda kutoka Mafinga kuja mjini Iringa.
Akisimulia kisa na mkasa wa askari
huyo kulewa chakali kiasi cha kushindwa kujitambua mmoja kati ya
wasamaria wema aliyejitolea kumshusha katika basi hilo alisema kuwa
askari huyo alipanda basi hilo Mafinga huku akiwa amelewa na wakati wote
wa safari alionekana akinywa pombe kali kiasi cha kushindwa kujimudu na
kuanza kutapika na kujisaidia haja ndogo ndani ya basi hilo.
Hata hivyo alisema baada ya kufika stendi ilikuwa ni vigumu kujitambua hivyo kupoteza fahamu na kulazimika kumpa msaada na kumzimua kwa maji kabla ya kupata fahamu kiasi na kujificha chini ya mfereji wa maji machafu .
Alisema kuwa mara baada ya kujitambua kiasi aliweza kutoa namba ya ndugu yake ambae ni askari wa FFU mjini Iringa aliyefika kumnusuru kuvuliwa nguo na kiongozi wake aliyefika eneo hilo na kumtukana akilishushia heshima jeshi kwa ulevi uliopitiliza
"Umelidhalilisha sana jeshi kwa askari kulewa hivi ukiwa katika sare, sasa nataka kukuvua sare kisha nakupeleka kulala polisi kabla ya kesho kukuchukulia hatua zaidi " alisikika akisema kiongozi huyo ambae jina wala cheo chake hakukitaja.
Maamuzi hayo ya kiongozi wake yaliwafanya mashuhuda kumuangukia na kumwomba amsamehe kwani bado ni kijana mdogo sana maombi ambayo aliyakubali na ndugu zake kumpakiza katika Taxi na kumpeleka eneo la Kihesa.