Kuwepo wa wageni katika shule hii kunavutia kwa muda umati mkubwa wa wanafunzi wa shule ya msingi inayopakana na shule hii.
Katika upande mmoja, baadhi ya
wanafunzi, wavulana kwa wasichana, wameketi na wanaonekana kujadiliana,
labda masomo yao, huku wale wa shule ya msingi wakiendelea kucheza
mchangani bila kujali.
Dakika chache baadaye, kengele
inakiriza kuashiria wakati wa kwenda nyumbani kwa wanafunzi wa shule ya
msingi na wakati wa kuendelea na masomo ya kibinafsi kwa wanafunzi wa
sekondari.
Lakini kwa kundi la wanafunzi wa kike wa shule hii, umewadia wakati wa kupokea mafundisho ila si ya kawaida waliozoea darasani.
Hata hivyo baadhi ya istilahi
wanazozisikia wakati wa mafunzo haya wamekumbana nazo katika somo la
Baolojia kwani ni mafunzo yanayohusu usafi na afya ya mfumo wa uzazi.
Darasa wanakosomea halina mwangaza
wa kutosha na joto ni jingi lakini hali hiyo haiwazui kumakinika ili
kufaidika kutokana na mafunzo hayo ya bure.
Baada ya kufahamiana, Rachael Ouko,
mwalimu wao kwa wakati huu, kutoka shirika lisilo la kiserikali la Femme
International, anaanza kikao kwa kuwauliza wanafunzi wanachofahamu
kuhusiana na miili yao na changamoto zinazowakabili kama wasichana.
Anapokea majibu tofauti ila hakuna
anayegusia donda ndugu kuhusu matatizo wanayokumbana nayo wanapokuwa
kwenye hedhi haswa njia za kujikinga ambazo ni changamoto kuu
inayowakabili maelfu ya wasichana kote nchini. Lakini Benta Oyugi,
mkufunzi mwingine katika kikao hiki anawakumbusha hayo.
Hiki ndicho kiini cha mafunzo ya
leo, anaeleza Bi Ouko, ingawa wasichana wanapokea mafunzo zaidi kuhusu
usafi wa miili yao na ugonjwa wa saratani ya kina mama.
Binti huyu anawavutia wasichana hao
kwa kuchomoa na kuwaonyesha makaratasi mawili yaliyochorwa mfumo wa
uzazi wa kina mama ambayo anadhamiria kutumia kutoa mafunzo yake.
Gharama ya sodo
Wasichana wote walio katika darasa
hili wametoka katika mtaa wa Mathare na Huruma ambako familia nyingi
zinaishi katika hali ya umaskini mwingi na huenda mafundisho na msaada
watakaopokea kuwa ya manufaa makubwa.
Kulingana na utafiti, idadi kubwa ya wasichana wanaoishi katika mitaa ya mabanda hawawezi kumudu gharama ya kununua sodo.
Takriban asilimia 65 ya wanawake na
wasichana nchini hawawezi kumudu gharama hii, suala ambalo limepelekea
wanawake na wasichana kutumia njia zingine kujikinga hedhi kila mwezi.
Njia hizi ni pamoja na kutumia
vipande vya nguo, makaratasi (ya vitabu na shashi), manyoya, godoro,
majani na njia zingine zilizo na athari mbaya ya kiafya.
“Changamoto kubwa kwa wanawake na
wasichana wanaoishi katika mitaa hii ni kwamba hawawezi kumudu gharama
ya sodo kila mwezi na ndiposa kuna haja ya kutafuta njia mbadala za
kuwasaidia. Idadi kubwa hawaelewi athari za kutumia baadhi ya njia
hizi,” asema Bi Ouko.
Asilimia kubwa ya wasichana katika
vitongoji duni katika miji tofauti nchini na mashambani hushiriki ngono
ili kupata pesa za kujikimu kimaisha ikiwemo kununua sodo kulingana na
utafiti.
Ikizingatiwa kuwa pakiti moja ya
sodo hununuliwa kati ya Sh60 na Sh80, bei ambayo kwa baadhi ya wanawake
hasa wasio na mapato makubwa ya kifedha, kuna haja ya kuibua njia mpya
za kuwapunguzia gharama wanawake, aeleza.
Na ndiposa shirika la Femme
International likishirikiana na Kampuni ya Ruby Cup limekuwa likitoa
bure vikombe maalum- vikombe vya hedhi, kwa wasichana na kina mama
katika vitongoji duni jijini Nairobi, Kisumu na Mombasa ili kuwasaidia
wakati wa hedhi.
Vikombe hivi kwa kiingereza
'menstrual cups’ vimewapunguzia gharama kubwa walionufaika kutokana na
mradi huo ulioanzishwa mwaka wa 2012.
“Nilianza kutumia kikombe nikiwa
kidato cha pili. Kimenisaidia sana kwa sababu kimeniondolea gharama ya
kununua sodo kila mwezi. Sasa naweka akiba pesa ya hizo,” aeleza Judith
Atieno, mkazi wa Huruma.
Kila mwaka, msichana mmoja ana uwezo
wa kutumia zaidi ya sodo 200 wakati wa hedhi, kumaanisha analazimika
kutumia pakiti kadha, ingawa kuna aina ya sodo ambazo zinaweza kuoshwa
na kuvaliwa tena.
Muda wa kudumu
Kulingana na Maxie Mathiessen mmoja
wa waanzilishi wa Ruby Cup, kikombe hicho kilichotengenezwa na silikoni
inayotumiwa katika matibabu kina uwezo wa kudumu miaka kumi.
Hii inamaanisha kuwa kwa muda huo wote, mtumiaji hatahitaji kununua sodo, jambo linalowapunguzia gharama ya maisha watumiaji.
“Kinaweza kutumiwa kwa masaa kumi na
mawili. Hii inamaanisha kuwa mwanafunzi anaweza kwenda shuleni bila
kuwa na wasiwasi wa kuchafua vazi lake,” asema Bi Ouko.
Kwa sababu hii wasichana
waliobaleghe wanaweza kuendelea na masomo yao bila kubabaika au
kushiriki katika ngono ya kulipwa ili kupata pesa za kununua sodo, asema
Amaia Arranz, Afisa Mkuu Mtendaji wa Ruby Cup, Afrika Mashariki.
Kikombe cha hedhi ni Sh1,800 humu
nchini na kinauzwa katika baadhi ya maduka ya rejareja na maduka ya
madawa kwa wale wanahitaji kukitumia.
Utafiti umebaini kuwa wasichana
wengi hasa kutoka familia maskini huacha shule wanapovunja ungo. Hii ni
kutokana na changamoto zinazowapata wakati huo wa maisha ikiwemo hofu ya
kuchekelewa shuleni.
Bi Atieno alisomeshwa na amezoea
kukitumia kikombe hiki ambacho kimekuwa sehemu ya maisha yake. Hata
hivyo mamia ya wasichana hawana ufahamu sio tu kuhusiana na matumizi ya
sodo bali pia afya ya uzazi na miili yao.
Hivyo mafunzo yanayotolewa siku hii
ni muhimu sana kwa wanafunzi na watumiaji wa vikombe, “Lazima kina mama
na wasichana wafunzwe jinsi ya kutumia kikombe hiki,” asema Dkt Caroline
Kabiru, mmoja wa watafiti waliofanya uchunguzi kuhusiana matumizi ya
vikombe vya hedhi kutoka Kituo cha Utafiti wa Watu Afrika (APHRC)
nchini.
Kikombe hiki 'huvaliwa’ au kutiwa
ndani ya njia ya uzazi mwanzoni mwa hedhi na kuna utaratibu maalum wa
kukitumia, aeleza Bi Ouko wakati wa mafunzo hayo.
“Hedhi hutona ndani mpaka kikombe
kinajaa au kinafikia sehemu fulani wakati ambapo mtumiaji anaweza
kukitoa na kumwaga damu kwa choo,” asema Bi Ouko. Aliwaonyesha wasichana
hao wa vidato vya pili na tatu utaratibu wa kuweka na kutoa bila
kutatizika.
“Kinaweza kuvaliwa kwa masaa 12.
Mtumiaji akitoa na kumwaga damu anafaa kukiosha halafu anakitia ndani
tena ingawa sio lazima kukiosha,” aeleza Bi Ouko.
Anaeleza kuwa wanawake wanaweza
kutumia karatasi ya shashi kupangusa kikombe chenyewe au wanaweza
kukitumia tena kilivyo, aeleza.
Kulingana na Dkt Kabiru, uchunguzi
umeonyesha kuwa kikombe hiki hakina madhara yoyote ya kiafya ila
mtumiaji anapaswa kunawa mikono kabla ya kukirejesha ndani. Usafi ni
kitu cha maana sana ili kuzima hatari ya kupata maambukizi ya maradhi.
Anaeleza mtumiaji anafaa vile vile kunawa mikono baada ya kukitoa.
Kuhifadhi
Baada ya hedhi kuisha huwa
kinachemshwa kwa dakika tano, sio kwa sufuria ya kupikia, lakini ndani
ya bakuli ya alumini iliyotengewa kazi hiyo.
Shirika la Femme International
huwapa wasichana ufadhili wa kikombe hicho, sabuni, bakuli na taulo ya
kujipangusa mikono baada ya kunawa.
“Kikombe hiki husaidia wasichana
kuweka siri wakati wa hedhi kila mwezi na pia huwasaidia kukaa wakiwa
wasafi,” asema Dkt Kabiru.
“Ni bora kikombe hiki kuliko kufua
vitambaa na kikasaidia wasichana wengi sana nchini ingawa sio kifaa cha
ajabu sana. Kinawapa wasichana nafasi ya kuchagua watakachotumia
kujikinga,” aongeza.
Lakini kwa wasichana wanaotoka kwa
familia maskini, kikombe hiki ni mwokozi kwani zaidi ya kuwa
kinawapunguzia hofu na aibu ya kila mwezi, kinawakinga kutokana na
athari za umaskini kama vile kushiriki ngono ya kulipwa na kuwapunguzia
wazazi wao gharama ya maisha.
“Kuna athari kubwa sana kwa
wasichana ya kutokuwa na uwezo wa kujikinga hedhi vyema kwa vile ni
ukiukaji wa haki zao. Ni kuwafedhehesha na kuwatesa,” limesema shirika
la Hanshep katika tovuti yake.
Mamia ya wasichana wa shule za
msingi na sekondari kutoka Mathare, Kibera, Kawangware, Dagoretti,
Kisumu na Mombasa wamefaidika kutokana na msaada huo.
swahilihub@ke.nationmedia.com