Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), imeandaa mdahalo maalumu wa Katiba utakaofanyika kesho kwenye Ukumbi wa Mlimani City ambao mzungumzaji mkuu atakuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Mwenyekiti wa taasisi
hiyo, Joseph Butiku alisema jana kwamba mdahalo huo wa amani ni kwa
ajili ya Watanzania wenye mapenzi mema na utakuwa wa wazi, ikiwa ni
sehemu ya kuziba pengo la mdahalo wa Katiba uliovunjika Novemba 2 ambao
ulifanyika kwenye Hoteli ya Blue Pearl.
Ulivunjika
baada ya kutokea vurugu zinazodaiwa kuanzishwa na kikundi cha watu kwa
lengo la kuvuruga uwasilishwaji wa ujumbe wa Katiba, huku Katibu wa
Uhamasishaji wa UVCCM, Paul Makonda akitajwa kinara wa vurugu hizo.
Siku moja baada ya vurugu hizo, Makonda alitumia muda mwingi kujisafisha kuwa alichokifanya ni kumkinga Jaji Warioba asidhurike.
“Tunasema
ni mdahalo wa amani na utakuwa wa wazi kwa watu wote wenye mapenzi
mema. Tuna mambo mengi ya kujadili, pia tunazungumza kuhusu maadili…
Tunaona namna watu wanavyojichukulia fedha za watu bila woga, mdahalo
huu unatupa fursa za kujadili kuhusu umuhimu wa Katiba kulinda maadili
ya viongozi na vifungu vingine muhimu,” alisema Butiku.
Aliongeza kuwa hiyo ni sehemu tu ya ushiriki wa mijadala na
midahalo ya umma kuhusu Katiba Inayopendekezwa, ambayo kwa sasa
inaendelea katika maeneo yote ya nchi, ikifanywa na viongozi wa kisiasa,
mashirika ya kujamii na hata watu binafsi katika vyombo mbalimbali vya
habari.
Alisema japokuwa sasa hivi wamepata ukumbi
mdogo unaoweza kuingiza watu 350, watatoa fursa kwa watu kuuliza maswali
na kupata majibu kuhusu vifungu na vipengele mbalimbali vyenye utata
vinavyoyahusu makundi yote ya kijamii ambayo yamepata uwakilishi katika
mapendekezo hayo ya Katiba.
Aliwataja wengine
watakaoshiriki kutoa mada kwenye mdahalo huo kuwa ni waliokuwa
makamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Butiku mwenyewe, Mohamed
Mshamba, Maria Kasonda, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Palamagamba
Kabudi na Humphrey Polepole.
Alisema midahalo hiyo ya
ndani ni sehemu tu ya mwendelezo wa mijadala inayoendeshwa na taasisi
hiyo iliyoanzishwa mwaka 1997 na kuzinduliwa na Rais wa Awamu ya tatu,
Benjamin Mkapa mjini Mwanza.
“Hawa vijana waliovuruga
mkutano wetu wa awali pale Ubungo Plaza, ambao ni vijana wetu na
tunawafahamu, hatutarajii kwamba watarudia tena vitendo vya kihuni kama
vile. Kimsingi hawana sababu kwa kuwa hawakunyimwa fursa ya kujadili na
kutoa mawazo yao, tulishawaonya,” alisema.