Pc Idd Makame(25) akiwa wodini
Kumetokea
tukio la aina yake katika mgodi wa madini ya almasi wa Mwadui uliopo
katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambapo askari polisi wa kikosi
cha kutuliza ghasia kutoka jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Pc Idd
Makame(25) amejeruhiwa vibaya mdomoni kwa kung’olewa meno sita baada ya
kupigwa jiwe kwa kutumia kombeo (kwa lugha ya Kisukuma Nh'ago) na
watu wanaodaiwa kuwa ni wachimbaji haramu wa madini katika mgodi wa
Mwadui wakati akitimiza wajibu wake wa kuhakikisha usalama wa raia na
mali zao
Tukio
hilo la kusikitisha limetokea Novemba 21,2014 saa mbili na robo usiku
katika eneo la Tanex katika mgodi huo wakati askari huyo akiwa na askari
wenzake wakiongeza nguvu baada ya askari wa kampuni ya ulinzi ya
Zenneth iinayolinda mgodi wa Mwadui kushindwa kuwadhibiti wachimbaji
wadogo wa madini maarufu "Wabeshi" waliotaka kuingia kwa nguvu mgodini
wakiwa na silaha za jadi.
Mashuhuda wa tukio hilo wameiambia Malunde1 blog kuwa kampuni ya ulinzi ya Zenneth Security Services Limited inayolinda
mgodi huo ilipata taarifa kuwa kuna wachimbaji haramu maarufu kwa jina
la Wabeshi waliotaka kuvamia mgodi huku wakiwa na silaha za jadi ikiwemo
mishale,mikuki,virungu,makombeo,mapanga na fimbo.
Kufuatia
hali hiyo askari hao wa Zenneth wakifika eneo la tukio kuwadhibiti
Wabeshi hao lakini ghafla walianza kushambuliwa kwa silaha za jadi.
Baada
ya kuona wanazidiwa nguvu,askari wa Zenneth walilazimika kuomba msaada
wa askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) cha jeshi la polisi mkoa
wa Shinyanga.
Baada
ya askari wa FFU kufika eneo la tukio nao walianza kushambuliwa na
Wabeshi hao ,ndipo PC Idd akapigwa jiwe mdomoni kwa kutumia kombeo na
kung’oka meno sita mdomoni na kukimbizwa katika hospitali ya mkoa wa
Shinyanga kwa ajili ya matibabu.
Mkurugenzi wa kampuni ya ulinzi ya Zenneth Security Services Limited Elisha Ndulu amethibitisha uwepo wa tukio hilo.
Naye
mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga Dkt Mfaume Salum
amesema Pc Idd alipigwa na kitu chenye ubapa mdomoni na kusababisha meno
sita kung’oka na anaendelea kupatiwa matibabu,hali yake inaendelea
vizuri.
Kamanda
wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alikiri kutokea kwa tukio
hilo na kuongeza kuwa tayari wanawashikilia watu wanne kwa mahojiano
zaidi na wanaendelea kufanya uchunguzi ili kuwakamata wahusika wengine.
Na Kadama Malunde-Shinyanga