Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono amelishwa sumu wakati
akiwa kwenye safari ya kikazi jijini London nchini Uingereza, imeelezwa.
Kwa
mujibu wa tovuti ya The Citizen, Mkono ambaye pia ni mwanasheria
maarufu, aliugua ghafla alipokuwa jijini humo.
Madaktari wake walisema kuwa alikuwa amelishwa sumu iliyokuwa imekusudiwa kuharibu figo zake ndani ya saa 72.
Madaktari wake walisema kuwa alikuwa amelishwa sumu iliyokuwa imekusudiwa kuharibu figo zake ndani ya saa 72.
“Ilikuwa siku mbili tangu niwasili London, nilianguka wakati nikifanya shughuli zilizonileta huku,” alisema na kuongeza:
“Nilijisikia vibaya na kupoteza kumbukumbu kwa takriban saa sita.”
Imeelezwa kuwa mbunge huyo alianza kutokwa jasho jingi ghafla kabla hajaanguka.
“Baada ya kuhudumiwa, madaktari wa London walisema sumu ilikuwa inaharibu figo yangu,” alisema.
Kwa
mujibu wa mbunge huyo, alikuwa ameonywa mapema kuwa muda mfupi kabla
hajasafiri kwenda London anapaswa awe mwangalifu, pia asifikie kwenye
hoteli zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kundi kutoka Tanzania, hivyo
aliamua kufikia kwenye makazi yake jijini humo.
“Nilipokea
meseji mbili kutoka kwa baadhi ya marafiki zangu wakinionya kuwa
mwangalifu wakati wote,” alisema na kuongeza kuwa: “Nilikuwa
nimeongozana na baadhi ya wabunge katika safari hiyo. Taarifa zinaeleza
kuwa maofisa usalama wa kikosi cha upelelezi nchini Uingereza wameanza
kulichunguza suala hilo.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema kuwa taarifa
kuhusu tukio hilo zilishafikishwa ofisi za Bunge ingawa hakuna
maelezo ya kutosha.
“Ninafahamu kuwa Mbunge Mkono
alipata matatizo ya kiafya wakati akiwa London, lakini anaendelea
vizuri…maelezo kuhusu ugonjwa wake unabaki siri kati ya Mkono na
madaktari wake,” alisema.
Mkono alikuwa mshauri mkuu wa
Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na Serikali dhidi ya Kampuni ya Kufua
Umeme ya IPTL na kwamba aliwahi kuziwakilisha kwenye Mahakama ya
Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) kabla ya mkataba
wake kumalizika mwanzoni mwa mwaka huu.
Tanesco
walikataa kusaini upya mkataba wa Mkono. Mbunge huyo anatajwa kuwa nyuma
ya kuvuja kwa kashfa ya Escrow, kutokana na taarifa nyingi anazoweza
kuwa anazifahamu kuhusu sakata hilo.
Julai mwaka huu,
Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo alimtuhumu Mkono kutumia
kashfa ya Escrow kumchafua, tuhuma ambazo Mkono anazikana.
Wiki
chache baadaye, Spika alimtaka Mkono kueleza namna ambavyo
aliishughulikia kesi ya IPTL na Standard Chartered Bank Hong Kong
iliyokuwa imefunguliwa dhidi ya Tanesco na Serikali.
Mkono
aliwasilisha taarifa kuhusu kuchotwa kwa Sh207 bilioni kwenye akaunti
ya Escrow kutoka Benki Kuu ya Tanzania wakati ambapo kulikuwa kuna kesi
nyingine inaendelea kwenye mahakama ya kimataifa.
Hatuwezi kuthibitisha kama kuna uhusiano wowote kati ya kulishwa
sumu na kashfa ya Escrow. Mkono amekuwa akisema kuwa uchunguzi pekee
ndiyo utakaoeleza ukweli.