Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini amekiri
kupokea Sh80.5 milioni kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engeering, James
Rugemalira akisema si mara yake kwa kwanza kupokea fedha kutoka kwa
mfanyabiashara huyo kwa kuwa mara nyingi huwa anachangia kwa uwazi
miradi ya jamii.
Askofu huyo alikuwa akizungumzia
Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iliyosomwa
bungeni juzi ikimtaja kuwa ni miongoni mwa viongozi wa dini na watu
wengine waliopokea mabilioni kutoka katika akaunti ya escrow.
Katika
ripoti hiyo, Zitto aliwataja viongozi wengine wa dini walioingiziwa
fedha katika Benki ya Mkombozi inayomilikiwa na Kanisa Katoliki kuwa ni
Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimanye
Simon (Sh40.4 milioni).
Akizungumza kwa simu jana,
Askofu Kilaini alisema Rugemalira hupendelea kuchangia kwa uwazi miradi
ya kijamii na si yeye peke yake aliyempatia mchango, bali kuna watu
wengine wengi ambao wameshampatia na kazi yake ni kuipokea na kuifikisha
sehemu husika.
Hata hivyo, kabla hajafafanua zaidi hoja yake, simu ilikatika na baadaye hakupatikana tena.
Hata
hivyo, jana askofu huyo alinukuliwa na Gazeti la Mawio toleo la jana
akisema fedha alizozipokea kutoka kwa Rugemalira ni kwa ajili ya miradi
mbalimbali inayoendeshwa na Kanisa Katoliki.
“Ndiyo
nimepokea fedha kutoka kwa James na hii siyo mara ya kwanza, kwani mara
nyingi amekuwa akichangia miradi mbalimbali ya kijamii,” alisema Askofu
Kilaini.
Alipotakiwa na gazeti hilo kuwataja wengine
waliochangia kanisa lake na kama nao wamechanga kutoka kwenye fedha za
akaunti ya escrow, alisema yeye hayumo kwenye michango hiyo.
Alipoulizwa
anawezaje kusema hayumo kwenye orodha ya waliopewa fedha kutoka akaunti
ya escrow wakati anakiri kuwa aliingiziwa mamilioni ya shilingi na
Rugemalira, alisema michango inayoletwa kwake haina siri, hivyo wezi
halisi ndiyo wakamatwe.
“Michango inayoletwa kwangu haina siri, shikeni wezi halisi,” alisema.
Askofu Nzigirwa
Kwa
upande wake, Askofu Nzigirwa ambaye alirithi kiti cha Kilaini, cha
Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam ameeleza kushtushwa kwake na
ripoti ya PAC iliyomtaja yeye na Kilaini kuhusika katika uchotwaji wa
Sh306 bilioni za escrow.
Hata hivyo, kiongozi huyo
alisema anaandaa taarifa itakayofafanua kwa kina namna ambavyo fedha
hizo zinazodaiwa zilitoka katika akaunti ya escrow zilivyoingizwa katika
akaunti yake pamoja na hoja na maswali mengi yanayoulizwa na wananchi
hasa waumini wa Katoliki kuhusiana na tuhuma hizo.
“Hizo
taarifa zimenishtua sana. Bado nashangaa inakuwaje mimi naambiwa
nimechota fedha kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow,” alisema
Nzigirwa alipokuwa akizungumza na gazeti hili jana.
Nzigirwa
alisema anachofahamu hadi sasa fedha zilizoingizwa katika akaunti yake
hazihusiki na escrow lakini atafanya uchunguzi ili kupata undani wa
fedha hizo na majibu yote yatakuwa katika taarifa atakayoitoa kwa vyombo
vya habari siku yoyote kuanzia leo