CHANGAMOTO kubwa inayoikabili sekta ya elimu nchini ya
ukosefu wa ubora wa elimu, imelifanya Baraza la Madiwani katika
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kuingia kwenye orodha ya Wilaya
zinazotarajiwa kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu nchini, baada ya
kupitisha azimio la kutaka maafisa elimu msingi na sekondari wilayani
humo kufanya usaili wa wanafunzi watakaofaulu kujiunga na elimu ya
kidato cha kwanza 2015 unafanyika ili kubaini kama wanajua kusoma na
kuandika au la.
Miongoni mwa maazimio yaliyoafikiwa na madiwani hao ni pamoja na madiwani kuamua kuwabana wazazi ambao
watashindwa kupeleka watoto wao shule na kujua idadi ya wanafunzi
watakaofaulu mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka huu ili waweze
kuhoji ufaulu wao ulitokana na nini kama hawajui kusoma na kuandika.
Imeelezwa kuwa, wakati wa maafikiano hayo baadhi ya
madiwani walikataa kuafiki mkakati huo kwa lengo la kuwalinda wakuu wa
shule za msingi walioruhusu watoto kufanya mtihani na endapo watafaulu
wakati wakijua hawajui kusoma wala kuandika.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina
yao wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, wameeleza kuwa ni
lazima maafisa elimu wote sekondari wahakikishe wanapata miongozo
kutoka Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Ufundi ya jinsi ya kusimamia zoezi
hilo kwasababu ndiyo kazi yao.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Sarah Dumba,
diwani wa kata ya Ludewa, Monica Mchilo, ameeleza kuwa siku maadhimio
hayo yalipoafikiwa haitasahaulika mashani mwake kwa yaliyotokea kutokana
na baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo kutaka kuwakumbatia wakuu wa shule
za msingi watakaobainika kuwa walifanya udanganyifu wa namna ya
kuwafaulisha wanafunzi huku wakijua kuwa hawana sifa stahiki.
Alisema chanzo cha maamuzi hayo ni baada ya kutathimini
hali ya taaluma katika Wilaya hiyo kuwa hairidhishi, na baada ya
kukatazwa kuwa wasizungumzie suala hilo baadhi ya wajumbe wa baraza
walijitenga.
Hata hivyo baada ya kufikishwa taarifa hiyo kwa bodi ya
wazazi, baadhi yao walipokea kwa furaha suala hilo, huku wengi wao
wakitaka umri wa wanafunzi kuanza shule uzingatiwe kwani wengi wa
wanafunzi wanaoanza shule za msingi wilayani humo wanachelewa kuanza
shule na kuwafanya kuwa na uelewa mdogo darasani na kushindwa kusoma
kabisa.
Baadhi ya wajumbe wa bodi ya wazazi wameeleza kuwa mkakati
wa madiwani hao hauna tatizo na kwamba tatizo la wanafunzi kushindwa
kusoma na kuandika linatokana na uongozi dhaifu kuanzia ngazi ya familia
hadi Wilaya ambapo walidai kuwa ukabila umeshamiri kwa walimu kujiona
kuwa kabila ama ukoo fulani haustahili kupata elimu iliyo bora.
Kwa upande wa Ofisi ya Elimu Msingi wilayani humo, imesema
kutokana na dhamira ya Baraza la Madiwani hao ni lazima kila mwanafunzi
atakayefaulu kujiunga na elimu ya kidato cha kwanza atafanyiwa usaili
huo. Pamoja na mambo mengine, imeelezwa kwamba usaili huo utasimamiwa na
walimu wakuu wa shule husika na kwamba mwanafunzi atakayebainika
kutojua kusoma au kuandika, atarejeshwa nyumbani.
via fikrapevu