WALIMU mkoani hapa wametakiwa kushirikiana na wazazi katika
kuwafundisha wanafunzi matumizi mazuri ya mitandao hususan simu za
mikononi katika mazingira yasiyoharibu maadili yao.
Akizungumza katika mahafali ya kuhitimu darasa la saba katika shule
ya Msingi Airport hivi karibuni, Katibu wa Uchumi na Fedha wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, Abdulikadri Mushi, alisema kuwa kwa sasa
Dunia iko katika kipindi cha utandawazi na watoto wadogo wako msitari
wa mbele kuharibiwa na utandawazi huo, kwani hutaka na wao kwenda na
wakati.
Alisema kuwa, sasa hivi watoto wadogo wanajua kutumia mitandao hasa
simu za mikononi na kompyuta na wengi hutumia kwa matumizi mabaya,
ambayo husababisha kujifunza na kuiga mambo mabaya.
“Utakuta watoto wanaangalia picha chafu kwenye simu zao, pia hata
kwenye kompyuta, kwani picha hizo zinapatikana kwenye mtandao,” alisema
Mushi.
Sambamba na hayo, Mushi aliahidi kujenga jengo la choo ili kupunguza
kero ya wanafunzi ya kuhangaika baada ya kilichokuwepo awali shule hiyo
kubomoka.
Naye Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Katubuka, Tatu Rajabu (CHADEMA),
alisema jukumu la kuhakikisha mtoto anakuwa katika mazingira mazuri
yenye maadili ni la mzazi pia walimu.
“Mzazi huachana na mtoto asubuhi na mtoto hushinda na walimu kwa muda
mwingi, hivyo walimu wawe na mzigo katika kuwafundisha na kuwaonya
watoto katika mambo ambayo hupelekea kuharibika kwa maadili,” alisema
Rajabu.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Wanajeshi Wastaafu, Nicas Bukobero, alisema kuwa kazi ya walimu ni
kuwafundisha na kuwalea wanafunzi katika maadili mema na sio kuwaacha
waharibiwe na utandawazi.