WATU wasiofahamika, usiku wa kuamkia jana wameandika maneno kwenye
kuta ukiwemo ukuta wa Kampuni ya Bakhressa katika maeneo ya Tazara
wakidhihaki Katiba Inayopendezwa sanjari na aliyekuwa Mwenyekiti wa
Bunge Maalumu la Katiba.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesema inafuatilia kubaini
watu wanaoandika maneno ya uchochezi kwenye kuta na kwamba wakigundulika
watashitakiwa kwa uchochezi na uvunjifu wa amani.
Miongoni mwa maandishi kwenye kuta hizo, yalitaka ipigwe kura ya
hapana kwa Katiba Inayopendekezwa na kwamba ni mbovu. Mengine
yalimshutumu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta.
Kamanda wa Polisi katika hiyo Maalumu, Suleiman Kova alisema
wanaendelea kuwatafuta ili kuweza kuwabaini na kuwafikisha mahakamani.
Alisisitiza jamii kutumia njia mwafaka ya kufikisha mawazo yao.
Alisema kwa kutoa maoni kwenye kuta hayana thamani, kwani hakuna atakayefanyia kazi lakini kwa kufuata taratibu yataheshimiwa.
Kutokana na maandishi hayo yaliyokutwa jana asubuhi, wafanyakazi wa
kampuni hiyo ya Bakhressa walilazimika kuyafuta kwa kupaka rangi upya
kwenye ukuta huo.
Mmoja wa vijana waliokuwa wakifuta maandishi hayo aliyejitambulisha
kwa jina moja la Hassan, alisema baada ya uongozi kupata taarifa ya
kuwepo maandishi hayo waliwataka kufuta na kupaka rangi upya.
Hivi karibuni, iliripotiwa kwamba mkoani Dodoma, maandishi kama hayo
yalikutwa katika ukuta wa ofisi za Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM).