MKAZI wa Manzese, Kata ya Mafiga,
Manispaa ya Morogoro, Oscar Philipo amemudu kuihudumia familia yake ya
watoto wawili kutokana na biashara ya kuokota na kuuza chupa tupu za
maji zinazomwingizia Sh 180,000 kila mwezi, imefahamika.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili
juzi katika banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ( NHIF) lililopo
ndani ya Uwanja wa Jamhuri wa mjini Morogoro mara baada ya kupima afya
yake, Banda la NHIF linatoa huduma za upimaji afya kwa wachezaji wa
Shimiwi na wananchi wa mkoa huo.
Katika mashindano ya Shimiwi
yanayoendelea kufanyika mjini hapa katika uwanja wa Jamhuri, Philipo
amekuwa akiokota chupa nyingi tupu za maji baada ya zinazotumiwa na
wachezaji.
Hivyo alisema, biashara ya kuokota chupa
tupu za maji aliianza miaka mingi na kwamba kazi hiyo imekuwa
ikimuingizia kipato cha kumudu kuendesha familia yake ya watoto wawili.
Mkazi huyo alisema, kutokana na tatizo
la ajira, ameamua kujiajiri mwenyewe kwa kuokota chupa hizo ambazo kwa
sasa zina soko kubwa Dar es Salaam na kwa siku ana uwezo wa kukusanya
kilo 20 na kilo moja inauzwa Sh 300 hivyo kujipatia Sh 6,000 kwa siku.
“Kwa kiwango cha kufikisha kilo 20 kila
siku ...ninapata makusanyo ya fedha Sh 180,000 kwa mwezi na zinanisaidia
kuendesha familia yangu, ingawa mahitaji ya kila siku ni makubwa kuliko
kipato kinachoingia,” alisema Philipo.
Hata hivyo alisema katika biashara hiyo
anapata changamoto hasa kutoka wa vijana wanaobwia 'unga' mitaani wakati
mwingine wanamkaba na kumwibia fedha.