Mzee wa miaka 62, Rashid Mbogo amepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Wilaya ya Mpanda kwa tuhuma za kumbaka mjukuu wake mwenye
umri wa miaka mitano.
Mtuhumiwa huyo, mkazi wa Kijiji cha Vikonge
kilicho katika Kata ya Mpandandogo wilayani Mpanda, alifikishwa mbele ya
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Chiganga Ntengwa na kusomewa mashtaka na
mwendesha mashtaka ambaye ni mkaguzi msaidizi wa polisi, Naathaniel
Silomba.
Ilidaiwa na mwendesha mashtaka huyo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Oktoba 19, mwaka huu saa 2:00 usiku akiwa nyumbani kwake.
Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa siku ya tukio,
mtuhumiwa akiwa anasubiria chakula cha usiku wakati kikiandaliwa na
mkewe, alimwita mjukuu huyo na kisha kumpakata mapajani. Alidai kuwa
baadaye alivua nguo na kuanza kumbaka huku mtoto huyo akipiga kelele za
kuomba msaada kwa kitendo cha babu yake.
Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa baada ya
kusikia mayowe hayo, bibi wa mtoto huyo na majirani waliingia ndani ya
nyumba na kumkuta mtoto sebuleni akiwa anatokwa na damu nyingi sehemu
zake za siri huku analia kutokana na maumivu makali aliyokuwa ameyapata.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa alikana mashtaka hayo ambayo alikuwa amesomewa na mwendesha mashtaka.
Hakimu Chiganga aliieleza mahakama kuwa dhamana ya mshtakiwa iko wazi endapo mshtakiwa atatimiza masharti.
Mshtakiwa alitakiwa awe na mdhamini mmoja mwenye mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh5 milioni.
Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana, hivyo alipelekwa rumande.