Shehena ya kemikali ya salfa iliyoachwa Kijiji cha Kifuru,
wilayani Kisararwe na Mamlaka ya Reli ya Tazara na Zambia (Tazara) baada
ya treni yake ya mizigo kupata ajali, huenda ikawa tatizo kubwa kwa
taifa kama itachelewa kuondolewa.
Tayari moshi uliotokana na moto uliozuka baada ya mabehewa hayo kupinduka umeshaanza kuleta matatizo kwa wakazi wa eneo hilo.
Baadhi ya wananchi ambao walizungumza na gazeti hili kijijini hapo
walisema kuwa kuungua kwa shehena hiyo kumewatia hofu kubwa kutokana na
kutambua kuwa kemikali hizo zina madhara makubwa kwa binadamu hasa
zinapoingia kwenye maji na kusambaa kwenye hewa. Kijiji hicho kina watu
571.
Aidha katika kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha, wananchi
hao wanahofu kwamba kemikali hiyo itaingia Mto Mpiji, ambayo maji yake
yanakutana na maji ya Mto Msimbazi ambayo yanatumiwa na wakazi wa Dar es
Salaam.
Baadhi yao walidai kupata madhara ya kiafya na kwenda kupata matibabu
katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe na kuelezwa kuwa hewa chafu ya
kemikali hiyo ndio iliyowasababishia madhara hayo na hivyo wakashauriwa
kunywa maji mengi pamoja na maziwa ili kuondoa sumu ya kemikali hiyo
mwilini.
“Baada ya moshi wa kemikali hiyo kutapakaa kijijini hapa, nilijisikia
vibaya mbavu zikaniuma, nilienda pale Kisarawe nikalazwa siku moja,
lakini madaktari waliniambia , tatizo langu limetokana na kuvuta hewa
chafu,” alisema Latifa Ramadhani.
Naye Mtendaji wa Kijiji cha Kifuru, Mohammed Kaudunde alisema baada
ya treni hiyo ya mizigo kuanguka wiki moja iliyopita alisema kijijini
hapo wananchi wengi walilalamika afya zao jambo ambalo liliwalazimu
kumuita daktari wa wilaya.
“Alikuja daktari wa wilaya hapa na timu yake wakatutangazia tu kwamba
tusisogee eneo la tukio na kwamba wananchi wanywe maji mengi pamoja na
maziwa,” alisema Kaudunde.
Alisema pia Katibu Tawala wa Wilaya na viongozi wengine wa
halmashauri ya wilaya walifika kijiji hapo na wananchi zaidi ya 20
wakalalamika kuathirika na moshi huo kiafya.
Mkuu wa Usalama wa Tazara, Elisha Mhoka alisema tayari Tazara
imeshawasiliana na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) ili kusafisha
eneo hilo.
Mhoka alisema NEMC walikuwa wanasubiri mafundi wa Tazara wamalize
kazi ya kutengeneza reli iliyokuwaimeharibika katika eneo hilo, kazi
ambayo wameikamilisha Ijumaa usiku ili waanze kazi hiyo ya kuondoa
shehena hiyo ya salfa.
“Wametuambia wakishaiondoa shehena hiyo na kwenda kuiteketeza, pia
udongo wa sehemu hii utachimbwa wote kuhakikisha udongo wote ambao
umemwagikiwa na kemikali hiyo unaondolewa eneo hili ili kulinda
mazingira ya sehemu hii,” alisema.
Alisema ajali hiyo imetokea eneo la mto na akaongeza kuwa kuna haja
ya kufanya usafishaji huo haraka kuhakikisha kuwa mvua zitakaponyesha
zisije zikasafirisha kemikali hiyo na kuipeleka kwenye visima vya asili
vya wananchi.
Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, Paschal Nkii
alipoulizwa na gazeti hili kama kuna wagonjwa ambao wamepelekwa
hospitalini hapo kutokana na tatizo hilo la kemikali, alikiri kulifahamu
tatizo hilo lakini akagoma kuzungumza kwa kuwa si Mganga Mkuu wa
Wilaya.
HABARILEO