Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kigezi
iliyoko Chanika, wilayani Ilala, Dar es Salaam (jina linahifadhiwa),
ameolewa na mkazi wa Mbondole, Halfa Ally (54) ambaye humfungia ndani
ili wakazi wa eneo hilo wasimuone.
Mama wa mtoto huyo, alisema jana kuwa alipata
taarifa kutoka kwa mdogo wake aliyekuwa akiishi eneo hilo kuwa mwanaye
anaishi na mwanaume huyo zaidi ya mwezi mmoja na nusu na huwa anamfungia
ndani ili asitoke nje.
Alisema mtoto huyo alikuwa anaishi na baba yake
mzazi kwa zaidi ya mwezi mmoja eneo la Kivule, alishangaa kusikia kuwa
mwanaye ameolewa na anaishi Mbondole.
“Nakumbuka ilikuwa Oktoba 7, mwaka huu tulitoa
taarifa kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa, tulishirikiana na wajumbe wa
kamati ya ulinzi wa mtaa huo ambao tulifika eneo hilo saa moja asubuhi
hadi saa 8 mchana na tulifanikiwa kumkamata mtuhumiwa,” alisema mama wa
mtoto huyo.
Alisema walishangazwa na kitendo cha mwenyekiti wa
serikali ya mtaa kumwachia huru mtuhumiwa bila kumchukulia hatua zaidi.
“Aliniambia tulimalize tu suala hili kienyeji ila niende duka la dawa nikanunue kipimo cha mimba ili tuangalie kama mtoto atakuwa kapata ujauzito na kama hana aendelee na shule.”
“Aliniambia tulimalize tu suala hili kienyeji ila niende duka la dawa nikanunue kipimo cha mimba ili tuangalie kama mtoto atakuwa kapata ujauzito na kama hana aendelee na shule.”
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Salum Matangula alikiri
kutokea kwa tukio hilo na alisema kilichotokea ni mtuhumiwa huyo alikiri
mbele ya kikao kuwa alipewa ruhusa na mama mzazi wa mtoto huyo aishi
naye.
Alisema kutokana na maelezo ya pande zote,
walibaini wote wana makosa ndipo walipomtaka mama huyo aende kwenye duka
la dawa ili achukuliwe kipimo cha mimba na baada ya hapo ampeleke
mwanafunzi huyo shuleni.
“Niliwaeleza kuwa wote wana makosa, mama alikuwa
anadai mwanaye akapime kwanza, nikamruhusu, lakini sijapata majibu hadi
leo,” alisema Matangula.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kigezi, Joseph Kalungutu
alisema mwanafunzi huyo ni mtoro na kipindi cha nyuma alikuwa
akihudhuria darasani mara moja moja na lakini kuanzia Septemba, mwaka
huu, hajaonekana kabisa shuleni.
“Mahudhurio ya mwanafunzi huyu ni mabaya, kuanzia
Mei 14, mwaka huu hakuingia darasani lakini ilipofika Juni alionekana
wiki moja, Julai alikuja siku mbili na Agosti aliingia darasani kwa siku
nne tu,” alisema.
Mwanafunzi huyo alisema waliishi na mwanaume huyo
kuanzia Septemba, mwaka huu, baada ya kuchukuliwa nyumbani alikokuwa
anaishi na baba yake mzazi eneo la Kivule.
“Alinichukua kama mke wake na kuniambia kuwa ninaenda kwake kumlelea watoto wake watatu ambao walikuwa hawana mlezi,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema hajapata
taarifa hiyo na kuahidi kufuatilia ili mtuhumiwa afikishwe kwenye vyombo
vya sheria.
Ally alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, alisema
ni kweli msichana huyo anamfahamu na alikuwa anaishi naye. “Sina cha
kukueleza zaidi ya hayo ninachofahamu huyo binti nilikuwa naishi naye,”
alisema Ally.
Na Pamela Chilongola, Mwananchi
Na Pamela Chilongola, Mwananchi