POLISI mkoani Rukwa wanamshikilia mkazi wa kitongoji cha Chanji,
Manispaa ya Sumbawanga, Magreth Juma (34) akituhumiwa kuiba mtoto wa
kike mwenye umri wa siku mbili ili asiachike katika ndoa yake, kwa kuwa
hajabahatika kumzalia mtoto mumewe.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob
Mwaruanda ambaye alisema uchunguzi wa awali umeonesha mwanamke huyo,
kabla ya kuchukua uamuzi wa kuiba mtoto, alishawahi kuzaa na mwanamume
mwingine kabla ya kuwa na mumewe wa sasa.
Hata hivyo, inadaiwa baada ya kuishi na mumewe wa sasa kwa zaidi ya
miaka miwili bila kupata mtoto mwingine, alihofia kuvunjika kwa ndoa
yake, hasa ikielezwa mumewe alikuwa akidai mtoto.
Mwaruanda alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitiwa nguvuni Oktoba 22, mwaka
huu asubuhi ikiwa ni muda mfupi tangu mtoto huyo aibwe kutoka kwa mama
yake katika kitongoji cha Bangwe.
Aliongeza kuwa awali alfajiri siku hiyo ya tukio, taarifa
ziliripotiwa Kituo cha Polisi Sumbawanga na mama mzazi wa mtoto huyo,
aitwaye Magreth Benias (28) kuwa mtoto wake mchanga amepotea katika
mazingira ya kutatanisha.
“Ndipo polisi kwa kushirikiana na raia wema walianza msako na muda
mfupi baadaye walimkamata mtuhumiwa akiwa na mtoto huyo nyumbani
kwake...tulibaini kuwa mama wa mtoto huyo na ndugu wa mtuhumiwa waliwahi
kuishi nyumba moja ya kupanga ambapo mtuhumiwa alikuwa akifika katika
nyumba hiyo kumtembelea ndugu yake,” alieleza.
Kamanda Mwaruanda alisema mtoto huyo aliyeibwa, amekabidhiwa kwa mama
yake mzazi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu wa afya yake.
Alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa awali wa
shauri lake kukamilika.
Na Peti Siyame, Sumbawanga
Na Peti Siyame, Sumbawanga