MANISPAA ya Kinondoni jijini Dar es Salaam itaweka kamera za CCTV
katika kituo kipya cha mabasi Simu 2000 kilichopo Ubungo.
Lengo la hatua
ni kurahisisha ukamataji wa wahalifu mbalimbali, wakiwemo wa
miundombinu iliyojengwa.
Mhandisi Mkuu wa manispaa hiyo, Baraka Mkuya alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumzia kuanza kutumika kwa kituo hicho.
Alitaka madereva wa daladala na abiria, kuwa waangalifu kwa matumizi ya miundombinu ya kituo hicho.
Mkuya alisema katika kuangalia usalama wa kituo hicho, Manispaa
imepanga kuweka kamera za CCTV, ambazo zitaweza kuhifadhi matukio yote
yanayotokea kituoni hapo.
“Kamera hizo zitakuwa zikisimamiwa na maofisa wa Polisi na
zitarahisisha upatikanaji wa matukio mbalimbali yanayoweza kujitokeza
kituoni hapo,” alisema Mkuya bila kufafanua zaidi hatua za uwekwaji wa
kamera hizo umefikia wapi.
Aliongeza kuwa ni vyema abiria kujifunza kutumia vyema miundombinu ya
kituo hicho, kilichojengwa kwa Sh bilioni 3.3 ili kiweze kudumu kwa
muda mrefu na kuwanufaisha watu wengi.
Kituo hicho kipya kinachukua nafasi ya kituo cha Ubungo Tanesco,
ambacho kimefungwa ili kutoa nafasi kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi
wa barabara za mabasi yaendayo haraka katika barabara ya Morogoro.
NA Lucy Lyatuu