Mwanafunzi
wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 13 wa shule ya msingi ya Themi
iliyopo jijini Arusha mkoani Arusha hali yake siyo nzuri baada ya
kubakwa na watu sita.
Tukio
hilo lilitokea majira ya saa 1 usiku Oktoba 7 mwaka huu katika kata ya
Daraja Mbili jijini Arusha. Imeelezwa kuwa sehemu yake ya kizazi
imeharibika kutokana na unyama huo.
Akizungumza
na mwandishi jana nyumbani kwake Daraja Mbili mara baada ya kuruhusiwa
kutoka katika Hospitali ya Kanisa Katoliki ya Father Babu ya jijini na
kuendelea na matibabu Hospitali ya Serikali ya Mount Meru Arusha
mwanafunzi huyo alisema pamoja na kuruhusiwa kutoka hospitali lakini
hawezi kutembea kutokana na maumivu makali yanayomsumbua.
Alisema
siku hiyo kulitokea ugomvi nyumbani na mama yake Zukhura Said (40) na
aliamua kukimbilia kwa mjomba wake ndipo njiani alipokutwa na dhahama
hiyo ambayo katika maisha yake hataisahau.
Mwanafunzi
huyo alisema alifanyiwa unyama huo karibu sana na nyumbani kwao na watu
waliomfanyia unyama huo anawafahamu kwa majina na sura na watatu
wameshakamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha na watatu bado
hawajakamatwa.
Mwanafunzi
huyo akizungumza alisema wakati akifanyiwa unyama huo alipoteza fahamu
na alijikuta asubuhi akiwa nje ya chumba cha mmoja wa watuhumiwa hao.
‘’Nimefanyiwa
unyama mkubwa sana nilipoteza fahamu kutokana na unyama huo na kwa
mujibu wa daktari kizazi changu kimetoboka shangazi yangu ndio aliyepiga
simu nyumbani kujulisha hali hiyo kwani alinikuta hapo nje asubuhi
majira ya saa 2 asubuhi’’, alisema mwanafunzi huyo.
Akizungumzia
tukio hilo mama mzazi wa mtoto huyo, Zukhura Said (40) alisema
anasikitishwa na jinsi upelelezi wa tukio hilo unavyoendeshwa kwani
mpelelezi wa tukio hilo {jina tunalo} amekuwa mstari wa mbele kutaka
wazazi wa pande zote wamalizane kwa kukaa mezani.
Mama
huyo alisema wahalifu waliosalia wako mtaani na wazazi wao kwa
kushirikiana na kiongozi wa mtaa {jina tunalo} wanafanya kila njama na
fitina kutaka kesi hiyo iondolewe Polisi na kurudishwa nyumbani.