Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka sita, jina linahifadhiwa
ameuawa kikatili kwa kujeruhiwa vibaya sehemu zake za siri baada ya
kunajisiwa, kisha kukatwa kichwani na watu ambao bado hawajajulikana.
Tukio hilo limetokea jana katika eneo la Mtaa wa
Saranga, wilayani Kinondoni na kusababisha vilio kutoka kwa baadhi ya
wanawake walioshuhudia mwili wa mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius
Wambura amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari
wamefanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa mmoja.
Alisema wanaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Mtaa wa
Saranga, Godwin Muro alisema mwili wa mtoto huyo uligundulika saa 2
asubuhi, baada ya wapitanjia kutilia shaka michirizi ya damu iliyoishia
porini.
“Juzi usiku nilipewa taarifa kwa njia ya simu
nikijulishwa kutoweka kwa mtoto huyo ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa
darasa la kwanza Shule ya Msingi Msingwa,”alisema Muro.
Alisema baada ya taarifa hizo alishukua hatua ya
kuwasiliana na baadhi ya viongozi wa mitaa iliyopo jirani naye, ili
kujua kama kuna mtoto atakuwa amekutwa katika maeneo baada ya kupotea.
“ Hakukuwa na jibu la matumaini hivyo
niliwajulisha polisi, ndipo asubuhi ya leo (jana) nilijulishwa kuna
michirizi ya damu, baada ya kufuatilia na kuingia ndani ya pori tukakuta
mwili wa mtoto ukiwa katika hali mbaya.”
“Wapo ambao wanaamini kwamba amekatwa baadhi ya
viungo kwenye sehemu yake ya siri, lakini nafikiri kwamba taarifa ya
uchunguzi wa kina itakayotolewa na polisi ndiyo itaeleza uhalisia wa
majeraha aliyopata mtoto huyo,” alisema Muro.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisema kwamba mapori
yaliyopo katika eneo lake, yamekuwa ni tishio kwa kuwa tukio hilo ni la
pili kukuta mwili ukiwa porini.
“Sasa haya mapori ni tatizo na tishio kubwa kwetu
hasa kwa watoto. Huyu ni mtoto wa pili kuna mwingine yule alikuwa wa
kiume alikutwa amekufa kwenye bwawa lililopo katika pori, tukiyagusa
wakubwa wanakuja juu,” alisema Muro.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI