Watu watatu wamefariki dunia na wengine zaidi ya 20 hawajulikani
walipo baada ya boti ya abiria iliyokuwa imebeba harusi kutoka Kibirizi
kwenda Kijiji cha Kigalye mkoani Kigoma kuzama katika Ziwa Tanganyika.
Ofisa Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Mkoa wa
Kigoma Maweni, Tatu Simba alithibitisha kupokea miili ya watu wawili
wakiwa wamefariki dunia na mmoja alifariki dunia muda mfupi baada ya
kufikisha hapo.
“Majeruhi ni kumi na moja wote wanawake 10 hali
zao ni nzuri na mmoja hali yake ni mbaya na kati ya hao waliofariki
wawili ni watoto na mmoja ni mtu mzima,” alisema Simba.
Naye manusura wa ajali hiyo, Rashid Jacob alisema;
“Boti ilibeba watu wengi sana kwani ina uwezo wa kubeba kama watu 35,
lakini tulikuwa kama 80 na ilizama baada ya mawimbi kutuyumbisha. Kuna
kama watu 10 au 20 wamezama na mtoto wangu wa mwaka mmoja hajaonekana.”