Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini ameapa kuzunguka nchi
nzima kuwahamasisha Watanzania kudai kufufuliwa kwa Taifa la Tanganyika
na kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.
Selasini alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki
katika sherehe za uzinduzi wa tawi la Chadema katika Kijiji cha Mande
wilayani Moshi Vijijini lililozinduliwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy
Owenya (Chadema).
Katiba inayopendekezwa ilipitishwa bungeni Oktoba
3, mwaka huu bila ya kuwapo kwa wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
“Tutazunguka nchi nzima na kitakachotuzungusha ni
kuwaomba nyinyi Watanzania kila mmoja awe mhubiri kwamba tunataka
Tanganyika yetu na Katiba yetu,” alisema Selasini na kuongeza:
“Katiba iliyopo siyo yetu, haibebi maoni yetu na
ikija kwetu kura yetu sisi itakuwa ni hapana kwa sababu katika Katiba
ile hakuna maoni yetu. Nawaomba sana tuhubiri hili”.
Selasini alisema tangu walipoamua kutoka katika
Bunge la Katiba Aprili 16, mwaka huu baada ya kuona maoni ya wananchi
yanafinyangwa, wamekuwa wakitaka maridhiano lakini wenzao Chama cha
Mapinduzi (CCM) hawakutaka.
“Tangu tumetoka tumekuwa tukishauri kwa sababu
Katiba siyo jambo la kulazimishana ni jambo la maridhiano. Tukawaomba
maridhiano lakini hawataki,” alisema na kuongeza:
“Nasema nchi hii wanaitumbukiza kwenye fujo na fujo zote duniani zimesababishwa na ubovu wa Katiba,” alisema Selasini.
Owenya alitumia ufunguzi huo kulaani tukio la
kukamatwa na kudhalilishwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa
Chadema (Bawacha), Halima Mdee.
Alisema kila Mtanzania anayo haki ya kuonyesha
kutoridhishwa na jambo fulani ambalo uamuzi wake ni wa kisiasa na moja
ya mambo hayo ni Katiba ambayo ni sheria mama ya nchi.
Mwishoni mwa wiki mwenyekiti huyo alitiwa nguvuni na polisi baada ya kuandamana bila kibali.