Binti wa miaka 20 aliyetambulika Riziki Haji mkazi wa Kijiji cha
Kondo mkoa wa Pwani, wilayani Bagamoyo, yupo kwenye mateso makali
kutokana na ugonjwa wa kifafa unaomsumbua kwa muda mrefu!
Riziki ambaye aliugua ugonjwa wa kifafa akiwa na umri wa miezi nane,
amekuwa akiishi katika mazingira magumu kiasi cha kufungiwa ndani usiku
na mchana.
Mtangazaji wa kipindi cha Hatua Tatu ‘Habari Ndio Hii’ cha 100.5
Times FM, Edson Mkisi Jr, alifika kijijini hapo na kushudia jinsi binti
huyo anavyoishi katika mazingira ya ‘kinyama na mateso’!.
Mkisi Jr alishuhudia sehemu anayolala binti huyo ikiwa katika
mazingira hatarishi kiasi kwamba yupo hatarini kung’atwa na wadudu wenye
sumu kali kama nyoka, ng’e ama tangu.
Aidha, imeelezwa kipindi cha mvua na baridi binti huyo huwa katika
hali mbaya zaidi kutokana na makuti yaliyotumika kutengenezewa kibanda
hayahimili hali hizo.
Akisumulia tukio hilo, jirani wa karibu na sehemu anayoishi Riziki
kwa sharti na kutoandika jina lake, alisema Riziki amekuwa katika maisha
mabaya kwa muda mrefu huku wazazi wake baba na mama wakitupiana mpira
mtu sahihi wa kuishi nae.
“Baba wa Riziki yupo Zanzibar na anafahamu vizuri sana hali ya mtoto
wake lakini wala hakuna msaada anaotuma….kuna muda mama yake aliamua
kumpelekea lakini siku chache baadae alimrejesha kwa mama yake! Lakini
pamoja na kumrudisha mama pia alimkataa na wasamaria wema wakamchukua na
kuishi nae,” anasema jirani huyo.
Jirani huyo alibainisha kuwa akiwa anaendelea na maisha kwa msamaria
huyo huku akionekana mwenye afya njema, alikuja bibi yake (mama mzazi wa
mama wa Riziki) na kumchukuwa na kwenda kuishi nae Bagamoyo ambapo siku
chache baadae alimrudisha kwa mama yake mzazi akidai ameshindwa kuishi
nae.
Akizungumza na Mkisi Jr, mama mzazi wa Rikizi, Bi. Asma Ramadhani,
alisema mtoto wake huyo awali alikuwa na afya njema lakini hajua
alipatwa na tatizo gani alipompeleka kwa baba yake Zanzibar.
Kuhusu kumfungia mtoto wake ndani saa 24, alisema analazimika kufanya
hivyo kutokana na hali yake huku akijitetea kwa kumuachia huru
husababisha matatizo zaidi hasa anapoanguka sehemu yenye mawe.
“Zamani nilikuwa namruhusu anakwenda hata kisimani lakini sasa simruhusu tena kutokana na hali yake,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kibanda anacholala, alisema kutokana na hali ya
Riziki anashindwa kumlaza na watoto wake wadogo hivyo kwa kuhofia
kuwalalalia watoto hao nyakati za usiku pindi kifafa kitakapomjia.
Hata hivyo, alikiri maisha ya mtoto wake anapolala si mazuri na kuahidi kumhamisha haraka iwezekanavyo.
Naye Juma Amani Pazi, mwenyekiti wa eneo hilo, mbali na kukiri
mazingira ya Riziki kuwa mabaya, pia alisema alikuwa hana taarifa kama
katika eneo lake kuna mlemavu anayeishi katika mazingira hatari kama
hayo.
CHANZO:TIMESFM