Abiria
zaidi ya 45 wengi wao wakiwa ni akina mama na watoto wa familia moja
waliokuwa wakienda harusini,wamenusurika kifo baada ya basi dogo la
abiria aina ya coaster la kampuni ya ''slim'' kushindwa kupanda mlima wa
kutoka tarafa ya soni kwenda jimbo la bumbuli wilayani lushoto na
kusababisha gari hilo kurudi nyuma kisha kwenda kugonga gema la barabara
na kusimama.
Wakizungumza katika eneo la tukio katikati ya mlima soni
wenye bonde kubwa lenye urefu wa mita zaidi ya 100 kwenda chini,baadhi
ya waathirika wa tukio hilo wameliomba jeshi la polisi kufanya ukaguzi
wa mabasi yanayofanya safari zake kutoka tanga kwenda katika maeneo
yenye miinuko kwa sababu kama lingerudi nyuma na kwenda kutumbukia
katika bonde lililopo pembeni mwa barabara hiyo hakuna abiria hata mmoja
ambaye angenusurika.
Kwa upande wao dereva na kondakta wa basi hilo linalofanya safari
zake kutoka jijini tanga kwenda jimbo la bumbuli wamesema ilitumika
akili ya ziada kusaidia kuokoa maisha ya abiria hao kwa sababu dereva
alijaribu kuweka gia namba moja lakini ilikataa ndipo alipoamua kukata
kona kali ili gari hilo liweze kwenda kulia kwake kwa lengo la kwenda
kugonga gema la barabara hiyo ili liweze kusimama.
Kufuatia hatua hiyo mkuu wa wilaya ya lushoto bwana majid mwanga
amewaagiza wamiliki wa vyombo vya usafiri wa magari ya abiria
kuhakikisha kuwa wanayafanyia ukaguzi magari yao kabla ya kusafiri kwa
sababu jiografia ya wilaya ya lushoto imezungukwa na milima na mabonde
hatua ambayo ni hatari kwa vyombo vya usafiri ambavyo ni vibovu.
CHANZO:ITV