SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi kudhibiti maandamano yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wafuasi watatu wa chama hicho wamefikishwa mahakamani jijini Dar es Salaam na wengine watano wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro.
Wafuasi
hao watano wa mkoani Morogoro wanashikiliwa na polisi wakidaiwa kupinga
agizo lilitolewa na viongozi wa jeshi hilo la kuwataka kutoandamana.
Wanachama
waliokamatwa ni pamoja na Witnes Makoyola (29), Katibu wa Chadema tawi
la Kiwanja cha ndege, Shukuru Makamba(46), Maria Lissu (28) mkazi wa
Kilakala na Katibu wa Baraza la Wanawake wilaya ya Morogoro Mjini,
Hussein Hassani (28) mkazi wa Mafiga na Odwin Peter (65) mkazi wa
Kiwanja cha ndege.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard
Paul alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 5:30 asubuhi
katika maeneo ya mtaa wa Konga.
Kamanda
Paul alisema Septemba 17 viongozi wa chama hicho waliandika barua ya
kuomba kuandamana, huku wakidai kuwa lengo la maandamano hayo ni kupinga
hatua ya wabunge wa Bunge la Katiba kuendelea na vikao huku wakijua
kuwa katiba haitapatikana.
Aidha
Kamanda Paul alisema kuwa barua hizo zilienda kwa wakuu wa polisi na
kwamba jeshi hilo lilizuia maandamano kutokana na taarifa za
kiintelijensia kuwa wapo baadhi ya wananchi walipanga kufanya uhalifu
wakati wa maandamano, ikiwa ni pamoja na kuwa kesi ya suala hilo bado
iko mahakamani.
Hata
hivyo, kamanda huyo alisema kuwa jeshi hilo liliwaita viongozi wa chama
hicho, lengo likiwa ni kuwazuia kuandamana ambapo alisema kuwa jana
majira ya saa 5:30 asubuhi katika maeneo ya mtaa wa Konga kulianza
kufanyika mkusanyiko wa watu wakijiandaa kuandamana baada ya kuweka
ulinzi katika maeneo yote waliyopanga kuanzia maandamano ya wafuasi wa
chama hicho.
Hata
hivyo, kamanda huyo alisema walifanikiwa kutawanya mkusanyiko huo kwa
kurusha mabomu ya machozi sambamba na kuwakamata watuhumiwa hao ambapo
alisema kuwa watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.
Kwa
upande wake katibu wa chama hicho mkoani hapa, Boniface Ngonyani
alisema kuwa maandamano hayo yaliyotarajiwa kufanyika jana majira ya saa
5.00 asubuhi yalizuiwa na jeshi la polisi ambapo jeshi hilo lilidaiwa
kuingia ndani ya ofisi za chama hicho na kuanza kupekua nyaraka na
kuzitwaa nyingine na kuondoka nazo.
Aidha
alisema baada ya hekaheka hiyo baadae wakabaini kwamba kompyuta mpakato
ya Mwenyekiti wa Chadema Wilaya, James Mkude pamoja na simu yake ya
mkononi havionekani.
Hata
hivyo, alisema kutokana na kukamatwa kwa wanachama hao ofisi ya Chadema
mkoa wa Morogoro tayari imewatuma wanasheria wake wawili ili kuweza
kufika polisi na kuangalia tatizo lililofanya kukamatwa kwa wanachama
hao.
Habari kutoka mkoani Dar es Salaam:
Wafuasi watatu wa Chadema wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuingia katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kinyume na utaratibu.
Wafuasi watatu wa Chadema wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuingia katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kinyume na utaratibu.
Wafuasi
hao ambao walifikishwa mahakamani hapo jana ni Ngaiza Kamugisha (28)
dereva, mkazi wa Vingunguti, Benito Mwapinga (30) Fundi nguo mkazi wa
Mtoni kwa Azzi Ally na Eliasante Bugeji (51) Mhasibu wa Hospitali ya
CCBRT mkazi wa Komakoma Kinondoni, Dar es Salaam.
Akisoma
hati ya mashitaka Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola akisaidiana
na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka na George Barasa, ambapo
alidai kuwa wafuasi hao wanakabiliwa na mashtaka matatu.
Mbele
ya Hakimu Mkazi Frank Moshi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Kongola
alidai mashtaka hayo ni kuingia kwa nguvu Makao Makuu ya Jeshi la
Polisi, kukaidi amri halali na kutoa lugha ya matusi.
Ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa Septemba 18 mwaka huu, washtakiwa waliingia
kinyume cha sheria ndani ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa hali ya
fujo.
Aidha,
ilidaiwa katika tarehe hiyo na maeneo hayo washtakiwa walikataa kutii
amri ya halali ya kutawanyika kutoka eneo la makao hayo ya polisi
iliyotolewa na Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Inspekta Zuhura, ambaye
alitoa amri hiyo baada ya kuruhusiwa na viongozi wake.
Akiendelea
kusoma mashitaka hayo, alidai katika kosa la tatu linalomkabili Bugeji
peke yake, inadaiwa akiwa katika mazingira ya Makao Makuu ya Jeshi la
Polisi alitoa lugha ya matusi kwa maofisa wa Polisi. Ilidaiwa maneno
hayo yaliyotolewa na mshitakiwa huyo yalikuwa yakiashiria uvunjivu wa
amani.
Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na upande wa mashitaka umeomba tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Wakili
wa wafuasi hao Peter Kibatala alidai mashtaka yanayowakabili washtakiwa
yanadhaminika, hivyo akaomba mahakama iwapatie masharti nafuu kwa
mujibu wa sheria.
Hata
hivyo, Kongola aliendelea kudai kuwa mahakama inatakiwa itoe masharti
yanayoendana na mazingira ambayo washtakiwa wametenda kosa hilo.
Kibatala
alidai kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhamana
ya washtakiwa ni haki yao na pia washtakiwa bado haijawatia hatiani, kwa
hiyo dhamana ni haki yao.
Hakimu
Moshi alisema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana wanatakiwa wawe na
wadhamini wawili wa kuaminika wakiwemo watumishi wa Serikali au
watumishi kutoka katika Taasisi inayotambulika wakiwa na barua za
waajili wao na vitambulisho vya kazi na wadhamini watasaini bondi ya Sh
500,000 kwa kila mmoja.
Kesi
hiyo iliahirishwa hadi Septemba 24 mwaka huu kwa washtakiwa kusomewa
maelezo ya awali na akaamuru washtakiwa warudishwe rumande kwa sababu
hawakuwa na wadhamini.
Mpaka
mwandishi anaondoka katika eneo la Mahakama washtakiwa walikuwa
hawajapata dhamana, ambapo kulikuwa na jitihada za kupiga simu Makao
Makuu ya Chadema ili wapate wadhamini.
Nje
ya mahakama Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Nickson Tugala alikuwa
aking'ang'ania kuingia mahabusu kuwaona washtakiwa, jambo ambalo
lilisababisha fujo katika eneo hilo.
Tugala
alionekana kubishana na Insepkta wa Jeshi la Polisi, Mussa Mkini mpaka
kufikia hatua ya kusogelea kwa karibu hali iliyowatia hofu watu
waliyokuwa katika eneo hilo kuwa watu hao wanataka kupigana.
Kutokana
na hali hiyo, ilimlazimu Mkini aombe nguvu kutoka Polisi na ilipofika
saa 6:10 mchana ziliingia gari mbili za polisi namba PT 1846 na PT 1145
zikiwa na askari wenye silaha za moto.
Mkini
alitoa amri ya Tugala kuchukuliwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi
cha Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na fujo ambazo alikuwa anafanya,
lakini bado Tugala alikuwa akiwagomea askari hao.
Baadaye
alikubali kuondoka nao, ambapo askari wawili walipanda kwenye gari
ambalo alikuwa akiendesha la M4C namba T 351 CAY. Askari mmoja alipanda
ndani ya gari na mwingine alipanda nyuma ya gari hilo wakiongoza kwenda
Central.
