Wanafunzi
wa darasa la awali Shule ya Msingi Nakayaya wakiwa darasani. Hata hivyo
shule hii haina chumba cha darasa la awali chumba hiki kimejengwa kwa
matumizi mengine na kwa sasa kinatumika kwa muda kwa kuwa kipo katika
ujenzi.
Mwalimu Christina Komba (kulia) wa darasa la awali Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko akiwa darasani.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo, Madina Mkali akizungumza na mwandishi wa habari hizi (hayupo pichani) ofisini kwake.
Mwalimu wa muda wa darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi akionesha baadhi ya nakala za vitabu walivyonavyo.
Tunduru
SHULE
nyingi za msingi zenye madarasa ya awali Wilayani Tunduru zimekuwa
zikiendeshwa kwa changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutokuwa na vitabu vya
baadhi ya masomo kabisa huku zikiwa na upungufu mkubwa wa vitabu kwa
masomo mengine.
Hali
hiyo imebainika hivi karibuni katika uchunguzi uliofanywa kwa baadhi ya
Shule za Msingi za Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma huku walimu wa
madarasa hayo wakielezea jitihada binafsi wanazozifanya kukabiliana na
changamoto hiyo.
Mwalimu
Christina Komba wa darasa la awali Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko
akizungumzia hali hiyo alisema darasa lake halina vitabu vya masomo
kama ya sanaa, Haiba na Michezo na wala miongozo ya namna ya ufundishaji
hivyo kila mwalimu anayefundisha darasa hilo hubuni nini afundishe
katika masomo hayo.
“Madarasa
ya elimu ya awali hayana vitabu, hayana miongozo…huwa tunaazima au
ukipata hela yako wewe binafsi unaenda kununua kitabu kimoja au viwili
ili uweze kuwasaidia watoto. Na baadhi ya masomo hayana vitabu kabisa
hata ukienda madukani katika Wilaya yetu vitabu kama Haiba na Michezo,
pamoja na Sanaa hazipo kabisa madukani,” alisema Bi. Komba.
Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Msingi Nanjoka, Batadhari Mkwela akizungumzia shule
yake alisema licha ya usajili wa wanafunzi wa awali kuongezeka kila
mwaka upatikanaji wa bajeti ya kuendesha elimu hiyo ni changamoto kubwa
huku uchangiaji kwa wazazi ikiwa wa kusuasua.
“…Darasa
la awali linahitaji vitendea kazi lakini havipo, hatuna vifaa kama
vitabu vya kutosha, nyenzo za kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa
hivi toka Serikalini, hatuna hata madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi
wa darasa hili,” alisema Mkwela.
Naye
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo, Madina Mkali alisema
uendeshaji wa darasa la awali shuleni hapo ni wa kusuasua kutokana na
kutokuwa na bajeti inayoletwa kusaidia elimu hiyo, isipokuwa kwa baadhi
ya mwaka kuletwa madawati kumi kwa ajili ya wanafunzi wa awali.
“…Uendeshaji
elimu ya awali hapa ni wa wastani kwa kweli kutokana na changamoto
zinazotukabili, kwanza vifaa vya kuwafundishia watoto hawa ni tatizo na
wazazi kwa eneo hili wamekuwa hawana mwamko wa elimu hii kabisa. Kwanza
hawachangii michango ya chakula kama inavyotakiwa ili mtoto apate
chochote awapo shuleni,” anasema mwalimu Mkali.
Kwa
upande wake mwalimu wa darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya,
Teckla Milanzi akitolea mfano shuleni hapo alisema vitabu vya Kiswahili,
Kiingereza, Sayansi na Hisabati kuna nakala moja moja tu kwa kila somo,
ambazo huzitumia yeye mwenyewe.
Aidha
mwalimu Milanzi aliongeza kuwa darasa hilo licha ya kuwa na changamoto
kedekede hata kwenye mgao wa fedha zinazoletwa shuleni kila mara halimo
jambo ambalo husababisha hali kuendelea kuwa mbaya zaidi.
Hata
hivyo mwalimu wa darasa la awali Shule ya Msingi Majengo, Hadija
Makamla alisema anavyo baadhi tu ya vitabu vinavyoitajika katika darasa
hilo, nakala ambazo pia ni chache ukilinganisha na ukubwa wa darasa
lake.
“…Ninazo nakala chache kwa ajili ya mwalimu tu ila wanafunzi
hawana hata kimoja…lakini kuna masomo mengine sina vitabu kabisa kama
vile Sanaa na Haiba ya Michezo sina kabisa hata mimi,” anasema mwalimu
Makamla.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na HakiElimu