Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es Salaam , tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalumu la Katiba. Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:
Tunaipongeza
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya maoni ya wananchi kuhusu
mabadiliko hayo na kutuletea Rasimu yenye maoni mengi ya Watanzania
bila kujali dini zao, upande wa Muungano walikotoka, hali zao za
kimaisha, jinsi na kabila.
Pia
tunaipongeza Tume kwa kuandaa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali kama
Randama, Nyaraka zenye maoni ya wananchi, picha, tafiti mbalimbali na
hata orodha ya watu walioshiriki kutoa maoni katika Tume.
Tume pia iliweza kuandaa tovuti iliyokuwa na kumbukumbu za Tume na maoni yote yaliyotolewa. Kazi hii ni ushahidi kuwa Tume iliandaa rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya wananchi.
Tume pia iliweza kuandaa tovuti iliyokuwa na kumbukumbu za Tume na maoni yote yaliyotolewa. Kazi hii ni ushahidi kuwa Tume iliandaa rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya wananchi.
Tume
imedhihirisha kuwa, ilitenda kizalendo na kwa mantiki hiyo, wajumbe
wote bila kujali vyama vyao, dini zao na upande wa Muungano walikotoka,
waliweza kujadili kwa uwazi na kweli na mwisho wakaridhiana katika kila
Ibara iliyopendekezwa. Hili linatufundisha kuwa Katiba ni maridhiano na
si jambo la masilahi ya kisiasa, bali ni suala la masilahi ya wananchi.
Tunaamini
kuwa kila mjumbe wa kamati ya kukusanya maoni ya wananchi aliheshimu
kiapo chake na hivyo kufanya kazi waliyokabidhiwa kwa uaminifu na
uadilifu na ya kwamba hawakushawishiwa au kupokea rushwa kutoka kwa
kundi, dini au chama chochote cha siasa wakati wa zoezi hili.
Baada
ya Tume kuwasilisha rasimu kwenye Bunge Maalumu la Katiba, Taifa
likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa wanadamu wapingao kweli kwa
uovu” (Warumi 1:18). Katika mijadala ya Bunge Maalum la Katiba (BMK)
yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya masilahi kwa wananchi, na
ukiukwaji wa sheria na kanuni. Mambo kadhaa yanadhihirisha hili:
Tovuti
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifungwa bila sababu za msingi
kutolewa wakati mchakato unaendelea. Hali hii imefanya zile nyaraka na
kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na kuwezesha mjadala wa
Rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga na ufahamu wa nyaraka hizo
kutowezekana kabisa.
Kwa
sababu hiyo, tumeona Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha
takwimu na taarifa mbalimbali ambazo wananchi hawawezi kuzipata kwa
ajili ya kuoanisha baina ya kinachojadiliwa bungeni na kilichomo katika
rasimu na viambatanisho vyake vyote. Tunajiuliza jambo hili limefanywa
na nani na kwa masilahi ya nani?
Bunge
la Katiba limeshindwa kusimamia kanuni kama ambavyo zilipendekezwa na
kuridhiwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. Kushindwa huku
kusimamia kanuni kumesababisha vurugu ndani ya Bunge Maalumu na
kumekwamisha matarajio ya wananchi kupata Katiba bora ya nchi yetu.
Matumizi
ya ubabe na wingi wa wabunge wa Chama Tawala (CCM), badala ya kanuni za
Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa Katiba kuhodhiwa na Chama
Tawala dhidi ya maslahi ya wananchi.
Mijadala
katika Bunge Maalumu la Katiba imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho,
ubabe na kupuuza hata kupotosha maoni yaliyotolewa na Wananchi kwa Tume.
Hali hii imelifanya Bunge Maalumu la Katiba kupuuzwa na hivyo kupoteza
heshima na hadhi yake.
Matokeo yake baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua kususia vikao vya bunge na wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa Katiba ni matokeo ya tendo la maridhiano na si suala la masilahi ya kikundi cha watu wachache.
Matokeo yake baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua kususia vikao vya bunge na wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa Katiba ni matokeo ya tendo la maridhiano na si suala la masilahi ya kikundi cha watu wachache.
Hatua
iliyofikiwa ni dhahiri, Mjadala wa BMK unaoendelea umeondoa kwa kiasi
kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano,
kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge,
ukomo wa ubunge, n.k., na kuwezesha maoni na masilahi ya chama tawala
kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na
uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba Mpya kwa nia ya
kulinda masilahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa
wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora.
Baada ya kujadili na kuona haya na mengine mengi, Jukwaa la Wakristo Tanzania lina maoni yafuatayo;
1.
Kwamba Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria) irudishe tovuti ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi
kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili Rasimu ya
Katiba kwa uwazi.
2.
Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauliwa na chama
tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea lijadili na
kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na siyo kufanya
mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.
3.
Kwamba mchakato wa Katiba usimamishwe ili kupisha majadiliano,
maelewano na maridhiano mwafaka, uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa.
Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977 yafanyike kuwezesha chaguzi
kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka kifungu kitakacholinda Rasimu
ya pili na kumtaka kiongozi ajaye kuendelea na mchakato wa Katiba.
4.
Kwamba baada ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza shughuli zake tena,
Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa
wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi katika Bunge la Katiba.
5.
Kwamba wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni yaliyoko katika
Rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa kinajadiliwa
kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni wakiwa na
uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba
inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa
nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni.
6.
Kwamba tunaomba Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe na kupewa mamlaka
kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza na kutoa
ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla hadi Katiba
Mpya itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi.
Jukwaa
la Wakristo Tanzania na Watanzania wote wanaoitakia nchi yao mema,
tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba amani ya nchi yetu sasa imo mikononi
mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya.
Tunakuomba
uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za
kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri
mshikamano, umoja na amani ya Taifa letu.
Ifahamike
kuwa wananchi wa Tanzania wako juu ya Wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi.
Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe wananchi wa Tanzania kuhamasishwa
kukikataa Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa tu chama hicho kimeyapuuza na
kimekataa maoni yao waliyotoa kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa
kufanya hivyo na viongozi wa nchi.
“Na
kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha
wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu
wa kila namna, uovu na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya,
wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri,
wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii
wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa
zao, wasio na rehema; si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”. (Rejea Warumi 1: 28-32)
Ikumbukwe
kuwa Rasimu ya Pili ya Katiba ni waraka halali na rasmi na ndiyo mawazo
ya Watanzania na tunahimiza kuwa Katiba ni ya wananchi na inahitaji
maridhiano na sio ubabe.
Imetolewa
na Tanzania Episcopal Conference (TEC) The Council of Pentecostal
Churches of Tanzania (CPCT) Christian Council of Tanzania (CCT) The
Seventh Day Adventists (SDA)
