UCHUNGUZI
wa awali kuhusu kupotea kwa ndege ya mizigo ya Shirika la Safari
Express ya nchini Kenya, umeonesha kuwa ndege hiyo yenye usajili namba
5Y SXP, aina ya Fokker 27, imepata ajali.
Taarifa
ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), iliyotumwa jana jioni
katika vyombo vya habari, imeonesha kuwa ndege hiyo iliyopoteza
mawasiliano juzi usiku, imeonekana ikiwa imeanguka katika eneo la
Kongetende Serengeti mkoani Mara.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, haijathibitika kama watu watatu
ambao ni wafanyakazi waliokuwa kwenye ndege hiyo, wamepoteza maisha au
la.
Awali,
Meneja wa Usalama na Usafiri wa Anga wa TCAA, mkoani Mwanza, John
Shushu alisema, ndege hiyo iliondoka kwenye Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Mwanza Agosti 31, saa 1.26 usiku.
Mawasiliano
ya mwisho na ndege hiyo, inayomilikiwa na Kampuni ya Safari Express ya
Nairobi Kenya, yalikuwa saa 2:05 usiku wakati ndege ipo umbali wa
kilometa 40 kutoka mpaka wa Tanzania na Kenya, ambapo ndege hiyo ilikuwa
angani futi 17,000 juu ya usawa wa bahari.
Ndege
ilipaswa kuvuka eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya saa 2:11 usiku,
lakini ilipoteza mawasiliano na Kituo Kikuu cha Kuongozea Ndege cha Dar
es Salaam na rubani wa ndege hiyo, hakutoa taarifa kuonesha iwapo ndege
yake ilikuwa na tatizo.
Baada
ya kubainika kwa mabaki ya ndege hiyo, uchunguzi wa ajali hiyo sasa
umeanza ili kubaini sababu ya ajali hiyo. Uchunguzi huo unashirikisha
wataalamu kutoka Mamlaka na Kitengo cha Uchunguzi wa Ajali.
