RAIS Jakaya Kikwete ametaka kuondolewa kwa mpango wa kuwalimisha wanafunzi ili waweze kupata chakula wakiwa shuleni kwani dhamana ya kumlisha mtoto ni ya mzazi na mtoto hatakiwi kujilisha mwenyewe.
“Dhamana hii lazima wazazi wabebe ili mtoto asilimie uji wake,” alisema Rais Kikwete. Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Kauli
ya Rais Kikwete ilikuja baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Fatma Ally kusema
wanafunzi wa shule za wilaya hiyo wamekuwa wakipata uji na chakula cha
mchana shuleni lakini baada ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani
(WFP) kujitoa kulisha uji shule zimelazimika kuwa na mashamba yao ili
kuwezesha watoto kupata uji wakiwa shuleni.
Rais
Kikwete alisema ni vizuri shule zikaanza kidogo kidogo kujitegemea kwa
wazazi kuchangia ili watoto waendelee kupata uji shuleni. “Mkianza kusema watoto wajilimie wenyewe itakuwa taabu walimu wataanza kushindana na watoto,” alisema.
Alisema watoto wa shule za msingi ni wadogo hiyo ni dhamana ya wazazi wao lazima watimize wajibu wao.
Alisema wakiachwa watoto walimie uji wao itakuwa ni shida kubwa kwa watoto, kwani watakuwa hawasomi ni majembe tu.
Alisema wakiachwa watoto walimie uji wao itakuwa ni shida kubwa kwa watoto, kwani watakuwa hawasomi ni majembe tu.
Ameitaka
halmashauri hiyo kuangalia namna ya kuwapatia uji wanafunzi wakiwa
shuleni ikiwa ni pamoja na wazazi kutimiza wajibu wa kuchangia chakula
kila baada ya mavuno, ili shule ziendelee kuwa na akiba ya chakula bila
kutegemea watoto kulima.
Awali
Mkuu wa ofisi ya WFP Mkoa wa Dodoma, Neema Sitta alisema mpango wa
kutoa chakula shuleni uko katika wilaya nne za Mkoa wa Dodoma ambapo
wanafunzi wa shule za msingi zaidi ya 400 wanafaidika nao.
Alisema,
siku za nyuma walikuwa wakitoa uji na chakula cha mchana, lakini baada
ya ufadhili kupungua waliamua shule zijitegemee kwa uji, lakini wao
wataendelea kutoa chakula cha mchana.
Alipohojiwa
na Rais Kikwete mpango wa chakula mashuleni utatolewa na WFP mpaka lini
alisema bado hajajua ni lini, lakini WFP imepunguza idadi ya shule
ilizokuwa ikizihudumia. Wilaya ya Chamwino ina jumla ya shule za msingi
110.
