STAA wa sinema za Kibongo, Salma Jabu 'Nisha', Jumanne
iliyopita alijikuta akizua taharuki kufuatia kuegesha gari lake nje ya
Hekalu la Freemason lililopo nyuma ya Hyatt Regency Dar es Salaam The
Kilimanjaro Hotel jijini Dar es Salaam.
Taharuki hiyo ilikuja pale Nisha alipoegesha gari lake eneo hilo na
kushuka kisha wanafunzi na watu wengine kusitisha shughuli na kumzunguka
kutaka kujua kulikoni staa huyo kufika eneo hilo linaloaminika kuwa
kila anayekwenda ni muumini wa imani ya Freemason.
Baadhi ya watu walimuuliza Nisha alichofuata kwenye hekalu hilo huku
mwenyewe akishindwa kujibu kwani alitupiwa maswali mfululizo.
Chanzo chetu kilidai kuwa msanii huyo baada ya kuona amezingirwa na
watu alisimama na kuzungumza nao kisha akabadili uamuzi, alirudi ndani
ya gari na kuondoka eneo hilo ambapo baadhi ya watu walidai huenda
alitaka kuingia kwenye hekalu hilo kama mastaa wenzake ambao mara nyingi
huonekana wakiingia na kutoka.
Kufuatia taarifa za chanzo hicho, gazeti hili lilimsaka msanii huyo
na kufanikiwa kumpata kwa njia ya simu ambapo alifafanua kuhusu suala
hilo."Aah! Dah, nyie habari hizo mmezipataje, mbona pale sijaona
mwandishi yeyote? Ukweli pale mimi nilipaki gari tu kwa ajili ya kufanya
mambo yangu maeneo yale lakini ghafla nikashangaa umati umenivaa, kila
mtu anataka kuniona laivu na kuongea na mimi.
“Wanafunzi ndiyo usiseme, sasa kutokanana na kusongwa na umati kama ule nikabadili maamuzi na kuondoka zangu,” alisema Nisha.
Kumekuwa na dhana miongoni mwa watu kwamba, baadhi ya mastaa wenye
mafanikio Bongo wamejiunga na imani ya Freemason huku ikisemekana
wanaishi kwa kuabudu kwenye hekalu hilo mara moja kwa wiki.
Hata hivyo, hakuna ushahidi wa moja kwa moja ni staa gani mwanachana
wa Freemason kwani hakuna aliyewahi kukiri kwamba yeye ndiye.
GPL
