Jalada namba KW/RB/7565/2014-SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI lililopo kwenye
Kituo cha Polisi cha Kawe, Dar, linamhusu mama aliyetajwa kwa jina moja
la Teddy, mkazi wa Tegeta kwa madai ya kumtumikisha na kumtesa mtoto
Magdalena Elisha (10) na kumsababishia majeraha na makovu ya vidonda
sehemu mbalimbali mwilini.
Habari kutoka ndani ya jeshi la polisi zilidai kwamba, Teddy
alimchukuwa mtoto huyo jijini Arusha kwa lengo la kumsaidia kukaa na
mwanaye kwa kuwa familia ya mtoto huyo haina uwezo na ameishia darasa la
tatu kwa kukosa vifaa vya shule.
Kwa mujibu wa Teddy, bila kujua kwamba ni kosa kumwajiri mtoto,
aliamua kumwadhibu mtoto huyo kutokana na kutomsikiliza bosi wake hasa
alipokuwa akionywa kuachana na tabia ambayo haikuwa ikimfurahisha.
Kwa upande wake Magdalena alidai kwamba alikuwa akipokea kipigo kila
siku hasa wakati mama huyo alipokuwa akirejea nyumbani kutoka ‘jobu’ na
kukuta mwanaye analia.
“Alikuwa akinipiga kila siku akikuta mtoto (wa miaka miwili) analia. Pia
kuna siku alinipiga sana asubuhi, nikaona nikimbilie kwa mjumbe, ndiyo
tukaenda kituo cha polisi, tukakutana naye akiwa anatoka polisi kutoa
taarifa kuwa nimepotea, mimi naomba nisaidiwe nirudi kwa mama yangu
Arusha,” alisema Magdalena na kumfanya bosi wake huyo apewe kibako na
vyombo vya sheria.
CHANZO: GPL
