CUF WALAANI WAANDISHI WA HABARI KUTEMBEZEWA KICHAPO NA POLISI

Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahimu Lipumba.

 Na Mwandishi wetu
CHAMA cha Wananchi (CUF) kinalaani vikali kitendo cha Jeshi la Polisi kuwapiga Waandishi wa Habari waliokuwa wakifuaitilia kuhojiwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahimu Lipumba alisema waandishi wa habari wanahaki za kupata habari lakini cha ajabu Jeshi la Polisi linawashambuliwa kwa kuwapiga kitendo ambacho ni unyanyasaji hakifai kufumbiwa macho.
Alisema pamoja na mapungufu makubwa ya katiba iliyopo Kifungu cha 18 (1) bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kutoa maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.
Alieleza katika rasimu mpya iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Warioba baada ya kupata maoni ya wananchi inaeleza Uhuru wa habari na vyombo vya habari katika kifungu cha 31 (1) kinaeleza kila mtu ana haki na uhuru wa  kutafuta, kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa.
Lipumba alisema katika kifungu hiko pia kinaeleza uhuru wa kuanzisha vyombo vya habari na njia nyingine za upashanaji wa habari bila kujali mipaka ya nchi na kwamba vitakuwa huru na haki ya kupata ,kutumia na kusambaza habari.
Pia alisema wanachama na wapenzi wa Chadema wana haki ya kujua hatma ya Mwenyekiti wao kuitwa na kuhojiwa Makao Makuu ya  Polisi na kwa hiyo wangemiminika kwa wingi katika eneo la kuhojiwa.
Alisema kuwapiga waandishi wa habari makao Makuu ya Jeshi la Polisi kunaonesha kutojali kabisa haki za binadamu katika nchi yetu. “Katika tukio ambalo Polisi wanajua linapigwa picha ungetegemea kwamba askari wangejaribu kulinda taswira ya jeshi la Polisi lisionekane waziwazi kuwa haliheshimu wala kujali haki za waandishi wa habari kufanya kazi yao. Ikiwa waandishi wa habari wanaweza kupigwa hadharani, je? Mwananchi wa kawaida, asiyekuwa na sauti kwenye gazeti wala radio na televisheni anafanywa nini anapokamatwa na polisi au kubambikiziwa kesi,”alihoji Lipumba.
Alisema hilo sio tukio la kwanza la kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandishi wa habari ambapo mwaka jana  mwandishi wa Habari wa Channel 10, Daud Mwangosi aliuawa na Polisi kwenye vurugu zilizotokea baada ya Polisi kuzuia shughuli za kufungua matawi za viongozi na matokeo ya Polisi aliyeongoza amepandishwa cheo.
Aidha alisema Jeshi la Polisi kwa kunyanyasa raia wa kawaida pamoja na waandishi wa habari ,wanasiasa wa vyama vya upinzani ni kutimiza maagizo ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyesema wapigwe tu ,hivyo alisema kwa kauli zake hizo hana sifa ya kuwa rais.
Alisema Chadema siyo chama pekee kilichotoa wito wa kufanya maandamano nchi nzima kuhusu jambo linaloendelea katika Bunge Maalum la Katiba na kwamba baada ya Rais Kikwete kutoa hotuba ndani ya Bunge Maalum la Katiba iliyopinga mambo muhimu ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Warioba ikiwa ni pamoja na mfumo wa muungano wa serikali tatu na kushutumu mapendekezo hayo kuwa yatasababisha Jeshi lipindue serikali, CCM walitangaza kufanya maandamano na mikutano nchi nzima kuunga mkono hotuba ya Rais Kikwete ambayo ilikuwa na kauli nzito za kichochezi.

Alisema lengo la kumuhoji Mwenyekiti Mbowe ni kumdhalilisha na kumtisha asiendelee kutimiza wajibu wake kama kiongozi wa juu wa chama  kitendo hiki ndicho kinachochochea  vurugu na fujo hivyo alilitaka jeshi kufanya kazi kama jeshi na si CCM.

Lipumba pia alilaani kitendo cha kuwazuia kufanya mikutano katika mikoa ya Lindi na Mtwara huku viongozi wa CCM wakiwa wanaendelea kufanya mikutano hiyo.
Hivyo basi alisema rais Kikwete anapaswa kuwa makini amalize mwaka wake wa mwisho vizuri na kwamba ubabe wa Polisi wa kuilinda CCM kwa kuzuia shughuli halali za vyama vya upinzani vitasababisha machafuko nchini.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo