Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege na kumwamuru kurejesha Dola za Marekani 42,543 (Sh68,068,800).
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi, Augustina
Mmbando alimtia hatiani Ekelege baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na
mashahidi saba wa upande wa mashtaka, vielelezo na ushahidi wa utetezi
uliotolewa na mshtakiwa.
Hakimu Mmbando alisema katika kesi hiyo, upande wa
mashtaka ulithibitisha mashtaka yote yanayomkabili Ekelege pasipo
kuacha shaka na kumhukumu kifungo hicho.
Mmbando alisema viongozi wapo kwa ajili ya kulinda
masilahi na rasilimali za nchi ili wananchi waweze kuifurahia keki ya
Taifa na siyo kufuata matakwa yao.
Alisema kiongozi kama Ekelege aliaminiwa na
kuteuliwa na Rais ili aweze kuiongoza TBS ambayo ni sehemu ya chanzo cha
mapato ya nchi, hivyo kuzembea kwake na kusababisha hasara ya kiasi
hicho cha fedha, hapaswi kuonewa huruma ili iwe fundisho kwa viongozi
wengine.
Katika shtaka la kwanza la kutumia madaraka yake
vibaya kwa kuziondolea asilimia 50 ya ada ya utawala, Kampuni za Jaffar
Mohamed Ali na Quality Motors, Ekelege alihukumiwa kifungo cha mwaka
mmoja jela.
Katika shtaka la pili la kuondoa ada za kampuni
hizo bila idhini ya Baraza la Utendaji kinyume na utaratibu wa TBS pia
alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na katika shtaka la tatu la
kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha alifungwa tena kifungo
kingine cha mwaka mmoja jela.
Hakimu Mmbando alisema vifungo hivyo vitakwenda
pamoja, hivyo mshtakiwa huyo atatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela na
kurejesha Sh68,068,800 anazodaiwa kulisababishia shirika hilo hasara kwa
uzembe.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mwendesha
Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth
Machulya alisema kwa kuzingatia uzito wa mashtaka aliyotenda Ekelege na
alivyoshindwa kuitumikia dhamana aliyopewa, anastahili adhabu kali ili
iwe fundisho kwa viongozi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Machulya aliiomba mahakama wakati ikifikiria kutoa adhabu kwa Ekelege izingatie sheria ya uhujumu uchumi.
Wakili aliyekuwa akimtetea Ekelege, Majura Magafu
aliiomba Mahakama impunguzie adhabu mteja wake kwa kuwa ni kosa lake la
kwanza, ana familia ya mke, watoto na wazee wanaomtegemea.
Utetezi wa Ekelege
Katika utetezi wake, Ekelege alikana kusababisha hasara kwa
kutoa msamaha, akisema hali hiyo ilitokana na udanganyifu uliofanywa na
kampuni husika.
Alidai kuwa kampuni hizo zilidanganya na
kusababisha kutoa uamuzi mwingine ambao haukuwa sahihi na bodi ya
wakurugenzi ya TBS ilipoitishwa iliridhia kuwa msamaha huo haukutolewa
kwa makusudi.
Alisema kwa kuwa TBS haikuwa na historia ya kutoa
msamaha hiyo na kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza na kampuni hizo hazikuwa
na uaminifu, aliiomba Mahakama imwachie huru.
Akijitetea, alisema kampuni ya Jaffar Mohamed Ali
ilipata msamaha baada ya kuwasilisha maombi yake ikidai kuwapo kwa
ushindani uliotokana na wakala mwenzake, Total Otomotive Services,
aliyekuwa akifanya mchezo mchafu wa kuvuta wateja kwa kutokagua viwango
vya ubora wa magari yao na kuwapa vyeti vya ubora.
Alidai kuwa menejimenti ya TBS iliijadili na
kukubaliana na matatizo hayo na ikatoa msamaha kwa kipindi cha Oktoba
2007 na Machi 2008 na alitakiwa kuanza kulipa tozo na gharama zake
ifikapo Aprili Mosi, 2008