Serikali inajipanga kufuta ada za sekondari, ili elimu kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne, itolewe bure.
Rais
Jakaya Kikwete, alisema hayo juzi katika mkutano wake na wanajumuiya ya
Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro, na wakazi wa vijiji vya jirani na
chuo hicho, katika ziara yake inayoendelea katika Mkoa wa Morogoro
iliyoanza Agosti 20.
“Sasa
hivi tunaangalia jinsi ya kufuta karo katika shule zetu zote za
sekondari za Serikali, ili kuhakikisha kila mtoto anayeanza darasa la
kwanza, awe na nafasi ya kumaliza sekondari kwa maana ya kidato cha nne,
bila kulazimika kuacha shule kwa sababu ya ada.
“Tunaangalia
kuondoa ada hii, ambayo wazazi wanalipa Sh 20,000 kwa shule za kutwa na
Sh 70,000 kwa shule za bweni, ili watoto wetu waingie darasa la kwanza,
na kwenda moja kwa moja hadi kidato cha nne bila wasiwasi wa
kukwamishwa na ada,” alisema Rais Kikwete.
Kwa
hatua hiyo, Rais Kikwete alisema mbali na kulenga kuinua elimu, pia
itawapunguzia mzigo wazazi na walezi wa watoto wanaosoma katika shule
hizo za sekondari za Serikali.
Alisema
zipo sababu za msingi zinazokwamisha wanafunzi wengi wa shule za
sekondari, kuendelea na masomo yao kutokana na wazazi wao kushindwa
kulipia karo ya shule, kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za
umasikini.
Rais
Kikwete alisema pamoja na kejeli nyingi zilizoelekezwa kwa shule za
sekondari za kata, kiasi cha kuitwa Yeboyebo katika miaka ya mwanzoni ya
shule hizo, bado zimekuwa na mafanikio makubwa, ambayo ni sehemu ya
mafanikio ya Sekta ya Elimu katika miaka karibu tisa ya uongozi wake.
Akielezea
historia ya kuanzishwa kwa shule za sekondari za kata, Rais Kikwete
alisema wakati alipokuwa akiingia madarakani, hali ya watoto kuingia
sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa mbaya.Kwa mujibu wa Rais
Kikwete, hali hiyo ilisababisha asilimia kati ya sita na kumi tu ya
wanafunzi waliomaliza darasa la saba, kusonga mbele kwa sababu shule za
sekondari zilikuwa chache.
“Kwa
miaka mingi, hatukujenga shule mpya za sekondari na kama mnavyojua,
Wakoloni wa Kiingereza ndio kabisa hawakujenga shule. Kazi hiyo
waliwaachia Wamisionari. Kwa hiyo wakati tunaingia madarakani, hali
ilikuwa mbaya ndiyo maana tukaja na Sera ya Shule za Kata,” alisema Rais Kikwete.
Alisema
takwimu rasmi zinaonesha kwamba, kulikuwa na shule za sekondari 1,745
mwaka 2005, zikiwemo shule 1,202 za Serikali na sasa ziko shule za
sekondari 4,576, zikiwemo shule 3,528 za Serikali.
Mafanikio
hayo ya kupanuka kwa sekta ya elimu, kwa mujibu wa Rais Kikwete,
yalileta changamoto hasa ya ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi.
Alisema Serikali imepambana na changamoto hiyo na zingine
zilizojitokeza, ambapo sasa wapo walimu karibu wa kutosha wa masomo hayo
kwa shule za sekondari zote nchini.
Mbali
na kusudio la kufuta ada, Rais pia alisema Serikali inaandaa utaratibu
maalumu utakaowezesha kujenga mabweni katika shule za msingi na
sekondari zilizopo maeneo ya jamii ya wafugaji.
Alisema
lengo ni kuwawezesha watoto wa jamii hiyo, waendelee kusoma hata pale
wazazi na walezi wao wanapohama kutoka eneo moja kwenda jingine kufuata
malisho ya mifugo yao.
“Tuna
tatizo kubwa katika eneo hili...watoto wengi wa wafugaji wanakatishwa
masomo kutokana na wazazi ama walezi kuhama kutoka eneo moja kwenda
jingine kufuata malisho...wanaohama wanaondoka na watoto wao wote na
kuwakosesha fursa ya kusoma,” alisema Rais.
Kuhusu
elimu ya juu, Rais Kikwete alisema kwa sasa kuna vyuo vikuu 51,
vikiwemo 15 vya umma na pia kuna ongezeko la fedha za mikopo ya elimu
kutoka Sh bilioni 16 mwaka 2005 na kufikia Sh bilioni 345 kwa sasa.
Mbali
na ongezeko la fedha za mikopo ya elimu ya juu, Rais Kikwete alisema
wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu waliongezeka kutoka
wanafunzi 16,000 mwaka 2005 hadi kufikia 95,000 kwa sasa.
Awali
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa, alipongeza
Serikali kwa kukuza mitaala ya wanafunzi wa vyuo vikuu na kushauri kuwa
ili wanafunzi washindane katika soko la ajira, upo umihimu wa mitaala
kuendelea kuboreshwa.
Alimwomba Rais Kikwete kusaidia kuboresha miundombinu mbalimbali ya chuo hicho kutokana na uchakavu wa majengo yake.
Naye
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Boniface Maiga, alitaja
changamoto kubwa zinazowakabili kuwa ni pamoja na uhaba wa sehemu za
malazi uliosababishwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaodahiliwa na
uchakavu wa miundombinu.
Alisema
licha ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), kutoa
mikopo hiyo kwa wakati, bado kuna malalamiko mengi kuhusu watoto wa
matajiri na wenye uwezo, ambao wameendelea kupewa mikopo.
Aliiomba serikali kufanyia utafiti suala hilo na ikibaini hali hiyo, fedha hizo zitolewe kwa watoto wengi masikini.