WANANCHI WAWATIMUA VIONGOZI WA CCM KWENYE MKUTANO WILAYANI RUNGWE

WANANCHI wa Kata ya Kambasegela wilayani Rungwe mkoani hapa, wamewafukuza viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM wa kata hiyo walipotaka kufanya mkutano wa hadhara ili kuimarisha chama chao.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mbeya, Fatuma Kasenga, Katibu wa jumuiya hiyo Kata ya Kambasegela, Frank Mwansasu, alisema wananchi walimtimua yeye na msafara wake kwa madai kwamba waliahidiwa maji zaidi ya miaka kumi sasa bila kupatiwa.

“Mwenyekiti, kero yangu kubwa ni kwamba, mimi na wenzangu tulifukuzwa na wananchi tusifanye mkutano wa hadhara wakati wa ziara yetu ya kata, wananchi wanasema waliahidiwa maji, lakini hawajapelekewa mpaka hivi sasa,” alisema Mwansasu.

Akijibu kero hiyo, Mwenyekiti Kasenga, alisema hayo ni matokeo ya baadhi ya viongozi kutowajibika vema katika nafasi zao.

Alisema suala hilo limemsikitisha, na kwamba yeye na msafara wake watalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi, ili kulipatia ufumbuzi.

Akiwa katika ziara hiyo, mwenyekiti huyo alipokea kero nyingine kwa baadhi ya wananchi wa Kata ya Nkunga, ambao walimwambia kuwa chama hicho kinachukiwa kwa udhaifu wa baadhi ya viongozi wake.

Wananchi walisema kata hiyo ina uhitaji wa umeme, na kwamba katika Kijiji cha Ibililo, kuna msigano wa viongozi, jambo ambalo linasababisha kutopatikana kwa maendeleo ya kijiji.

“Jitokezeni kwenye marekebisho ya daftari la kudumu la mpiga kura na ukifika wakati wa uchaguzi, wazee, vijana na wanawake wanaofaa wapeni nafasi wagombee,” alisema Kasenga.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo