Polisi wa kituo kidogo cha polisi Usalama kilichopo maeneo ya Bunju A Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam jana usiku walilazimika kufyatua mabomu ya machozi pamoja na risasi kutawanya kundi kubwa la wananchi waliokuwa wamekizunguka kituo hicho kwa madai ya kutaka kuwachukuwa watuhumiwa wanaoadaiwa kukutwa na shehena ya viungo vya binadamu.
Tukio hilo lililoibua hofu kubwa miongoni mwa wananchi wa maeneo hayo
 na jiji la Dar es Salaam kwa ujumla, lilitokea majira ya jioni mara 
baada ya wananchi kushuhudia gari ndogo aina ya Suzuki Carry, ikiwa 
imebeba viungo hivyo ambavyo vinakadiliwa kuwa vya watu zaidi ya 100.
Awali,  kulisambaa taarifa kuwa katika eneo la dampo Mpiji kuna 
viungo vya binadamu ambapo wananchi walitoa taarifa katika kituo cha 
polisi Usalama ambapo ufuatiliaji wa tukio hilo ulianza mara moja kabla 
ya kukamatwa kwa gari hiyo.
“Awali tulikwenda kule dampo kwa ajili ya kutupa takataka lakini 
tuliona viongo vya binadamu tukaja kutoa taarifa polisi na muda mfupi 
tuliiona ile gari iliyomwaga viungo hivyo ikipita tena kwenda kumwaga 
vingine na ndipo tulipoifuatilia na bodaboda na baadae kukamatwa na 
polisi.” Alisema shuhuda wa tukio hilo.
Wakaendelea kutabanaisha kwamba, mara baada ya kuona wamezingirwa 
baadhi ya watuhumiwa walikimbia na kumwacha dereva ambaye alikamatwa na 
polisi wa kituo hicho cha Bunju A.
Mwanahabari wetu ambaye alifika eneo hilo la tukio muda mfupi tangu 
kutokea kwa tukio, alishuhudia umati mkubwa wa wananchi wa rika 
mbalimbali wakiwa kituoni hao kwa lengo la kushuhudia tukio hilo.
Akizungumza na  waandishi wa habari, Kamanda 
wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambara, amethibitisha 
kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kwamba jeshi lake limekamata viungo
 hivyo vya binadamu na kwamba tayari wamevipeleka katika hospitali ya 
Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Viungo hivyo vimepatikana…Kumepatikiana gloves, kuna visu 
ambavyo vinatumika mara nyingi katika shughuli mbalimbali za 
kioparesheni. Viungo hivi ambavyo ni pamoja na miguu, mikono, kuna 
mafuvu ya vichwa. Kuna mbavu, kuna vitu ambavyo tunadhani inawezekana ni
 mioyo na vingine ni mapafu. Kwa hiyo tunavichukua na kuvipeleka kule 
kwenye hospitali ya Muhimbili. Sasa uchunguzi zaidi utafanyika kuanzia 
hapa.”
Bofya  hapo  chini  Kumsikiliza

