Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga.
Wingu zito limegubika kifo cha mke wa askari polisi wa wilayani Mwanga, Kilimanjaro aliyefia chumbani kwa dereva wa bodaboda.
Uchunguzi 
wa awali wa polisi unadai kuwa mwanamke huyo alilala chumbani huko usiku
 mzima wa kuamkia Jumapili, siku ambayo maiti yake iligunduliwa saa 12 
jioni. 
Uchunguzi huo pia unadai kuwa mtuhumiwa ndiye aliyempigia simu shangazi ya mwanamke huyo na kumuita nyumbani kwake kwa dharura.
  
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
 alisema jana kuwa baada ya shangazi kufika, alishuku jambo baada ya 
kuona mtuhumiwa anaweweseka bila kumweleza alichomwitia.
  
“Akiwa amesimama nje ya chumba cha huyo bodaboda 
ambaye alionekana kama mlevi hivi, aliona kwa ndani kukiwa na mwanamke 
aliyekuwa amelala sakafuni,” alisema na kuongeza kuwa shangazi huyo 
aliamua kusukuma mlango ndipo alipomkuta mtoto wa kaka yake akiwa 
amelala sakafuni.
  
“Shangazi aliita majirani na katika hekaheka hiyo 
polisi waliitwa na kukuta mwanamke huyo akiwa amekufa na ndani ya chumba
 kulikuwa kumezagaa paketi za pombe,” alisema.
  
Mtuhumiwa anashikiliwa na polisi wilayani Mwanga 
huku taarifa ya chanzo cha kifo hicho zikisubiri uchunguzi wa mwili wa 
marehemu.
